Msichana,12,atoweka baada ya kusombwa na maji Kangemi

Mwanafunzi wa darasa la 6 Ashley Nyaboke na mamake walikuwa wamelala usingizi mzito

Muhtasari
  • Juhudi za kumwokoa msichana huyo hazikufua dafu kwani maji hayo yalizidi kuvunja kuta kabla ya kumfagia yeye na kila kitu kilichokuwa ndani ya mto.
Crime Scene
Image: HISANI

Msichana wa umri wa miaka 12 alisombwa na maji huku mafuriko yakisababisha uharibifu katika sehemu tofauti za nchi, na kusababisha mamia ya familia kuhama makazi.

Juhudi za kumwokoa msichana huyo hazikufua dafu kwani maji hayo yalizidi kuvunja kuta kabla ya kumfagia yeye na kila kitu kilichokuwa ndani ya mto.

Mamia ya kaya pia ziliathirika kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Jumatano jioni usiku wa kuamkia leo jijini Nairobi na maeneo mengi nchini.

Karibu saa kumi na moja asubuhi Alhamisi, wakazi wa Waruku eneo la Kangemi jijini Nairobi waliamshwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa iliyonyesha jijini.

Mwanafunzi wa darasa la 6 Ashley Nyaboke na mamake walikuwa wamelala usingizi mzito nyumba yao ilipofurika na kuvunja kuta kabla ya kumfagia hadi kwenye mto ulio karibu.

Shughuli ya msako iliyoanza saa kumi na mbili asubuhi Alhamisi iliendelea kwa muda lakini ilitatizwa na mvua kubwa iliyoshuhudiwa baadaye alasiri.

Familia hiyo imeiomba serikali kusaidia kupata mwili wa binti yao.

Mafuriko hayo yalifagia zaidi ya kaya 100, katika eneo hilo.

Wakaazi walioathiriwa ambao walipoteza bidhaa za thamani ya maelfu ya pesa sasa hawana mahali pa kuita nyumbani.

Mafuriko yatatiza usafiri katika baadhi ya barabara.