Rais Ruto achukua mikopo 8 ndani ya miezi 4

Mikopo hii italipwa kati ya mwaka wa 2030 na 2047

Muhtasari

• Hazina inaeleza kuwa mikopo hiyo itatumika kugharamia miradi ya maji, usalama wa chakula, afya ya uzazi, uboreshaji wa sekta isiyo rasmi na Biashara Ndogo na za Kati (MSMEs).

RAIS WILLIAM RUTO
Image: KWA HISANI

Utawala wa Kenya Kwanza tayari ilipokea mikopo minane  ya thamani ya shilingi bilioni 43.4 katika muda wa miezi minne, kati ya Septemba 1 hadi Desemba 31.

Hazina ya kitaifa inasema mikopo mipya iliyotiwa saini kati ya serikali ya Kenya, na wakopeshaji italipwa kati ya mwaka wa 2030 na 2047.

“Jumla ya thamani ya mikopo minane iliyosainiwa ni sawa na  shilingi bilioni 43,381, 450,293. Miwili kati ya mikopo hiyo ilikuwa imetolewa wakati wa kuwasilisha ripoti hii,” Njuguna Ndungu, waziri wa fedha aliambia wabunge. 

Serikali ya Rais Ruto inategemea mikopo ya masharti nafuu kugaramia mikopo ghali ya muda mfupi ambayo imekuwa mzigo kwa walipa ushuru. 

Hazina inaeleza kuwa mikopo itatumika kugharamia miradi ya maji, usalama wa chakula , afya ya uzazi, uboreshaji wa sekta isiyo rasmi na Biashara Ndogo na za Kati (MSMEs).

Hazina ilikopa Shilingi bilioni 16.7 kutoka kwa  Shirika la maendeleo la kimatifa  ili kuongeza ufikiaji endelevu na usimamizi wa maji ya ardhini katika mipaka ya Pembe ya Afrika.

Serikali pia ilikopa Shilingi bilioni 2.7 kutoka Mizuho Bank Europe NV ambazo zitatumika kwa vifaa vya matibabu vya Turnkey na kandarasi za ukarabati wa vifurushi ili kuboresha vitengo vya uzazi na watoto wachanga .