DP Gachagua na mkewe wavunja kimya baada ya kukamatwa kwa Mackenzie na Ezekiel

Alivishauri vyombo vya sheria na amri kufuata utaratibu wa kisheria kumchunguza na kutenda haki.

Muhtasari
  • Mchungaji Dorcas alibainisha kuwa nchi inaongozwa kwa sheria, na wahalifu wanapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa katiba.
Mama Dorcas Gachagua
Mama Dorcas Gachagua
Image: Facebook

Mke wa naibu Rais Mchungaji Dorcas Rigathi mnamo Alhamisi, Aprili 27, alitoa wito wa kushtakiwa kwa kasisi  Paul Mackenzie, ikiwa atapatikana na hatia ya kutenda makosa yoyote kama mshtakiwa.

Mchungaji Dorcas alibainisha kuwa nchi inaongozwa kwa sheria, na wahalifu wanapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa katiba.

Hata hivyo, alilitetea kanisa , akisema kwamba kesi hiyo inapaswa kushughulikiwa kando na kelele za kubana makanisa na mashemasi, kwani huenda Mackenzie alitenda kwa hiari yake mwenyewe.

"Ikiwa Paul Mackenzie ni mhalifu, anapaswa kutendewa kama mtu binafsi. Hata familia yake haipaswi kuwa sehemu ya uhalifu wake. Paul Mackenzie sio kanisa. Kwa kweli, amesema yeye si mchungaji, lakini ni Bw. Paul," alisema katika hafla ya kuadhimisha wajane huko Kibra, Nairobi.

Alivishauri vyombo vya sheria na amri kufuata utaratibu wa kisheria kumchunguza na kutenda haki.

“Hatuwezi kusimama pale na kusema kwa sababu Mkristo mmoja amenaswa katika mazingira ya maelewano, mwili wote wa Kristo ulaumiwe, mhalifu ni mhalifu, gaidi ni gaidi, muuaji ni muuaji.

"Wachukuliwe kwa njia ya sheria na washtakiwe kama wana hatia. Wawekwe gerezani."

Hapo awali, Naibu Rais Rigathi Gachagua alitetea kanisa kufuatia kukamatwa kwa wachungaji Mackenzie na mwenzake mwenye utata, Ezekiel Odero.

Akizungumza wakati wa mkutano na viongozi wa sekta mbalimbali, Gachagua alionya dhidi ya kukashifu kanisa  kwa sababu ya vitendo vya viongozi wachache wa kidini.

"Kesi ya Kilifi ilionyesha kuwa, kama sehemu nyingine yoyote ya jamii, hata kanisa lina watu wasiofaa. Lakini hatuwezi kulaani kanisa zima kwa sababu ya shughuli za wachungaji wawili au watatu," Gachagua alisema.