Mhubiri Ezekiel Odero akamatwa kwa madai shughuli kanisani mwake

kulikuwa na madai ya vifo vilivyoripotiwa kwenye kanisa lake.

Muhtasari

• Alikamatwa siku moja baada ya kuhojiwa kwa muda mrefu kwa madai kuwa kanisa lake pia linajihusisha na uchawi.

Mhubiri Ezekiel Odero wa kanisa la New Life Prayer Picha: CHARLES MGHENYI
Mhubiri Ezekiel Odero wa kanisa la New Life Prayer Picha: CHARLES MGHENYI

Mwinjilisti Ezekiel Odero wa Kituo cha Maombi cha New Life Prayer Center na Kanisa amekamatwa kwa madai ya mahubiri ya itikadi kali kwa umma.

Alikamatwa siku moja baada ya kuhojiwa kwa muda mrefu kwa madai kuwa kanisa lake pia linajihusisha na uchawi.

Kamishna wa kanda ya Pwani Rhodah Onyancha alisema mhubiri huyo alikamatwa katika eneo la Mavueni, kaunti ya Kilifi.

Alisema hii ni kwa sababu kulikuwa na madai ya vifo vilivyoripotiwa kwenye kanisa lake.

Pia aliamuru kufungwa kwa Kituo cha New Life Prayer na Kanisa.

“Analetwa Mombasa kuhojiwa. Taarifa zaidi zitatolewa,” alisema.

Kwa sasa yuko Makao Makuu ya Polisi Pwani.

Mhubiri huyo alikanusha madai ya uchawi katika kanisa lake mbele ya makachero wa Kilifi siku ya Jumatano.

Polisi wanaofahamu matukio hayo walisema hatua ya kumwita Jumatano ilichochewa na ufukuaji unaoendelea wa miili kutoka shambani katika Msitu wa Shakahola.

Shamba hilo linahusishwa na mchungaji Paul Mackenzie wa Good News International Church.

Kufikia sasa zaidi ya miili 95 imefukuliwa kutoka kwenye makaburi katika msitu huo, maafisa walisema.