Watu 17 waokolewa kutoka kanisa la itikadi potovu Nakuru

Polisi waliwapata wakiwa wamezuiliwa katika nyumba moja ambayo ni ya mwanamke mwenye kanisa lisilosajiliwa kwa jina 'Army Rurwama'.

Muhtasari

• Kulingana na ripoti ya polisi, mzazi kutoka Kaunti ya Uasin Gishu aliripoti kuwa bintiye alikuwa amefungiwa katika nyumba mojaNakuru.

Polisi Jumamosi waliwaokoa watu 17 kutoka kwa kanisa linaloshukiwa kuwa la mafunzo ya kupotosha huko Nakuru.

Kulingana na ripoti ya polisi, mzazi kutoka Kaunti ya Uasin Gishu aliripoti kuwa bintiye alikuwa amefungiwa katika nyumba moja katika kijiji cha Kamwene 'B', wadi ya Kihingo na Kaunti Ndogo ya Njoro.

"Polisi wakiongozwa na OCS wa kituo cha polisi cha Ndeffo walitembelea eneo la tukio katika kijiji cha Kamwene 'B' katika kaunti ndogo ya Njoro kaunti ya Nakuru na kubaini kuwa amepata kazi ya Uuguzi wa Afya ya Jamii katika zahanati ya GK ya Nigeria," taarifa hiyo ilisoma.

Polisi walisema kazi hiyo ilikusudiwa kwa bintiye mwenye umri wa miaka 35 ambaye ni mama wa watoto wanne.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mwanamke huyo alitakiwa kuripoti Aprili 26, 2023, lakini alikataa na kusafiri na mumewe hadi kijiji cha Kamwene ‘B’.

Polisi waliwapata wakiwa wamezuiliwa katika nyumba moja ambayo ni ya mwanamke anayeshukiwa kuendesha kanisa lisilosajiliwa na linaloshukiwa kuwa la itikadi potovu linalojulikana kama 'Army Rurwama'.

Wote waliokolewa na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Njoro kwa uchunguzi zaidi. Wale 17 wanasemekana kufanyiwa maombi na kufunga.

Watu hao 17 waliokolewa huku kukiwa na uchunguzi kuhusu kifo cha zaidi ya watu 100 katika msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Kufikia sasa polisi wamewazuilia Wachungaji Ezekiel Odero na Paul Mackenzie wanaodaiwa kuwafunza wafuasi wao na kusababisha vifo hivyo.

Idadi ya waliofariki katika Shakahola sasa imefikia 108 katika uchunguzi wa itikadi potovu ambao umelishtua taifa na kusababisha wito wa kukandamizwa kwa vikundi vya kidini.

Polisi wamewahamisha baadhi ya wafuasi wa Mchungaji Ezekiel wa New Life Prayer Centre na Kanisani hata uchunguzi ukiendelea.