Aliyekuwa MCA wa Antubetwe Kiongo George Kaliunga ameuawa katika shambulizi la ujambazi kaunti ya Meru.
Alitangazwa kufariki alipofika katika Hospitali ya Maua Jumapili jioni baada ya kupigwa risasi kifuani.
Kaliunga alikuwa ameandamana na maafisa wa polisi waliofuata mifugo yake iliyoibwa katika wadi hiyo iliyoko eneo bunge la Igembe Kusini.
MCA huyo wa zamani alipigwa risasi Kinna, Kaunti ya Isiolo alipokuwa na maafisa wa polisi kutoka Meru.
Walikuwa wakifanya ufuatiliaji wa mbuzi wake 71 waliokuwa wameibiwa.
Mkuu wa polisi wa Mutuati William Letting alisema mbuzi hao walikuwa wameibiwa kutoka kwa marehemu huko Malaene.
“Tuliviziwa tukiwa tunawafuata kwa kutumia nyayo zao, Kaliunga alipigwa risasi kwa sababu alikuwa mbele yetu,” alisema.
Mkuu huyo wa polisi alisema majambazi hao waliondoka baada ya mazungumzo mafupi wakimkimbiza MCA huyo wa zamani hospitalini.
Mbunge wa Igembe Kaskazini Julius Taitumu amewapa pole familia ya marehemu Kaliunga.
Taitumu alisema kifo cha Kaliunga kimegusa watu wengi na kuonyesha jinsi visa vya ukosefu wa usalama na wizi wa ng'ombe vimeongezeka huko Meru.
"Wacha Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki ajue kwamba hatujastarehekea au kufurahishwa na kile kinachoendelea haswa katika eneo bunge la Igembe Kaskazini," Taitumu alisema.
Haya yanajiri takriban wiki moja baada ya wafugaji wawili kuuawa kwa kupigwa risasi na mwingine kujeruhiwa vibaya katika eneo bunge la Mutuati, eneo bunge la Igembe Kaskazini.
Mgambo wa serikali ya kaunti ya Meru pia aliuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akiwafuata wezi wa mifugo huko Isiolo.