Mapema Jumanne polisi katika kaunti ya Kilifi walitangaza kufanikiwa kumtia nguvuni mke wa mchungaji mwenye utata Paul Mackenzie ambaye amekuwa akitafutwa kwa muda.
Kulingana na taarifa zilizopo, mke wa Mackenzie alikamatwa katika eneo la Mtwapa ambapo amekuwa akijificha tangu msako dhidi ya waumini wanaohudhuria mafunzo potovu ya Mackenzie katika shamba lake la ekari 800 huko Shakahola yang’oe nanga.
Kulingana na Nation, Rhoda Mumbua Maweu alikamatwa pamoja na shangazi yake Jumatatu, Mei 1 usiku. Vyombo vya usalama vimemtambua Mumbua kama mshiriki wa kanisa baada ya jina lake kutajwa wakati wa uchunguzi.
Alikuwa amepewa kazi kama meneja wa rasilimali kwa watu wa kanisa, na polisi katika uchunguzi wap wanachimbua Zaidi kutaka kujua kuhusu jukumu lake katika kanisa ambalo sasa limetajwa kuwa dhehebu lenye itikadi potofu.
Kulingana na jarida hilo, Maafisa wa upelelezi kutoka DCI wamepata ushahidi ambao umewapa imani kwamba alikuwa muhimu katika usimamizi wa kanisa na alihusika katika mafundisho potofu yanayoshirikiwa kanisani.
Polisi wameripotiwa kupitia rekodi za simu za Mackenzie na kupata jumbe za ndani kati yake na mkewe. Walidai kuwa Mumbua alihusika katika kusajili wanachama wapya katika dhehebu hilo na huenda alikuwa na udhibiti wa taarifa nyeti za kifedha.
Mumbua ni mke wa tatu wa Mackenzie baada ya mke wa kwanza kufariki mwaka wa 2009, akiacha watoto wawili na wa pili 2017, akiacha watoto wanne.
Jumatatu shughuli ya upasuaji wa maiti 110 iliyofukuliwa katika shamba la Shakahola iliongozwa na mwanapatholojia mkuu wa serikali Johansen Oduro ambaye ripoti yake ilitupilia mbali wizi wa viungo vya mwili na kusema kwamba wengi wao walifariki kwa kukosa nguvu mwilini kwa njaa.