logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Raila atoa matakwa mapya kabla ya mazungumzo na Kenya Kwanza

Raila anataka kuachiliwa kwa wana azimio waliokamatwa kwa kushiriki maandamano.

image
na Radio Jambo

Makala04 May 2023 - 13:39

Muhtasari


• Kiongozi wa Azimio pia alisisitiza matakwa yake ya awali kwamba mazungumzo yakamilishwe ndani ya siku 30 yatakapoaanza.

Odinga amtambua Ruto kama rais

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga ametoa matakwa mapya kabla ya kurejelewa kwa mazungumzo ya pande mbili na wenzao wa Kenya Kwanza.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Alhamisi, Raila alisema miongoni mwa matakwa mapya ni kwamba mchakato wa mazungumzo lazima upanuliwe ili kujumuisha washiriki nje ya Bunge ili pawepo ushirikishwaji wa makundi mengine.

"Bado tunaamini mazungumzo hayawezi kuendeshwa kikamilifu na kwa njia ya kipekee kupitia mchakato wa bunge. Lazima kuwe na njia ya kujumuisha na kuruhusu ushiriki wa washiriki kutoka nje ya Bunge katika mazungumzo," Raila alisema.

Alisema muundo wa aina hiyo utaunda mwanya wa kujumuisha masuala mengine ya kikatiba ambayo hayajakamilika kuchunguzwa katika mazungumzo hayo.

“Tumewaagiza wajumbe wetu kuzungumzia hili,” Raila alisema.

Kiongozi wa Azimio pia alisisitiza matakwa yake ya awali kwamba mazungumzo yakamilishwe ndani ya siku 30 yatakapoaanza.

Raila ameendelea kusema kuwa vijana wote ambao wako korokoroni kwa madai ya kushiriki maandamano ya Azimio lazima waachiliwe kabla ya kurejelewa kwa mazungumzo.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alisema Jumanne kwamba takriban watu 46 walikamatwa wakati polisi wakishika doria ili kudhibiti maandamano yaliyopangwa na Azimio.

"Pia tumeweka wazi kuwa vijana wetu waliokamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za uwongo lazima waachiliwe bila masharti kabla ya mazungumzo."

Raila alisema wafuasi wa Azimio waliokamatwa Jumanne wamelaumiwa kwa machafuko yaliyosababishwa na wahuni wa kukodiwa.

Alisema matakwa yao mengine kwa serikali ya Kenya Kwanza bado hayajabadilika wanapojipanga kwa ajili ya kuanza kwa mazungumzo ya pande mbili. Hii ni pamoja na kupunguzwa kwa gharama ya maisha, ukaguzi wa matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2022, urekebishaji na uundaji upya wa tume ya IEBC na kukomesha kuingiliwa kwa usimamizi na utendakazi wa vyama vya kisiasa kwa nia ya kuvishirikisha serikalini ili kudhoofisha. 

Madai hayo mapya yanajiri saa 24 baada ya Azimio kusitisha maandamano makubwa ya Alhamisi ili kutoa fursa kwa mazungumzo.

Ilifuatia uamuzi wa Kenya Kwanza kumtoa mbunge wa Aldas Aden Keynan kutoka kwa timu yao ya mazungumzo.

Kujitoa kwake kulikuwa ni sharti ambalo Azimio ilikuwa imetoa kwa wao kusitisha maandamano tena.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved