Wabunge wa Bungoma wataka Yesu wa Tongaren aachiliwe

Aliongeza kuwa Yesu wa Tongaren hakuwasilisha madhara yoyote, akisema alikuwa mtu aliyelenga kuombea watu.

Muhtasari
  • Wakiongozwa na mbunge wa Tongaren John Chikati, wabunge hao waliongeza kuwa kuachiliwa kwa mhubiri huyo hakufai kujumuisha masharti ya dhamana.
Yesu wa Tongaren
Image: HISANI

Baadhi ya wabunge kutoka Magharibi wametaka kuachiliwa kwa mhubiri anayeishi Bungoma Eliud Wekesa, almaarufu Yesu wa Tongaren.

Wakiongozwa na mbunge wa Tongaren John Chikati, wabunge hao waliongeza kuwa kuachiliwa kwa mhubiri huyo hakufai kujumuisha masharti ya dhamana.

"Na tunauliza ya kwamba atolewe bila masharti yoyote. Asipatiwe bond yoyote atolewe on free bond

Aliongeza kuwa Yesu wa Tongaren hakuwasilisha madhara yoyote, akisema alikuwa mtu aliyelenga kuombea watu.

 

"Anaombea Papa wa Roma akuwe rais. Yesu wa Tongaren aachiliwe."

Chikati alisema mhubiri huyo ni maskini ambaye hawezi kuhusishwa na utakatishaji fedha.

Aliongeza kuwa alikuwa akifahamiana vyema na Yesu wa Tongaren, ikizingatiwa kwamba walikuwa wakiishi eneo moja.

Chikati aliandamana na Mbunge wa Webuye Mashariki Martin Wanyonyi.

Mnamo Mei 10, Yesu wa Tongaren alijiwasilisha kwa kituo cha polisi kuhojiwa baada ya kuitwa na kamanda wa polisi wa Bungoma Francis Kooli.

Kooli alimuita kiongozi wa kanisa la New Jerusalem kuhojiwa kuhusu mafundisho ya kidini yanayodaiwa kutiliwa shaka.

Mnamo Mei 11, Mahakama ya Bungoma iliruhusu mahakama kumzuilia kwa siku nne zaidi kwa uchunguzi wa kiakili na kukamilisha uchunguzi.

Anashutumiwa kwa uendeshaji kinyume cha sheria wa jamii isiyosajiliwa, itikadi kali, na utakatishaji fedha.

Haya yanajiri siku moja baada ya Kiongozi wa wasio amini katika uwepo wa Mungu nchini Kenya, Harrison Mumia ameitaka Huduma ya Kitaifa ya Polisi kumwachilia huru kiongozi wa Kanisa la New Jerusalem Church lenye makao yake mjini Bungoma Bw Eliud Wekesa almaarufu Yesu wa Tongaren mara moja pasi na shuruti yoyote.

Katika taarifa, Mumia kupitia chama chao cha wakana Mungu Kenya, walitoa changamoto kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi kuwasilisha Yesu halisi mahakamani ikiwa wanataka kesi yao dhidi ya Yesu wa Tongaren isimamishwe.

"Tunadai kuachiliwa mara moja kwa Yesu wa Tongaren. Ni lazima polisi wamtoe Yesu halisi ikiwa dai lao ni kwamba mtu huyu si Yesu Kristo halisi, Mwana wa Yahwe!” AIK ilisema katika taarifa iliyotiwa saini na kiongozi wake Harrison Mumia.

Kulingana na Mumia, Yesu wa Kibiblia ni mhusika wa kubuniwa, aliyebuniwa na dini zinazodai kuwa za Kikristo, tofauti na Yesu wa Tongaren ambaye yuko katika maisha halisi.