Dereva aliyekuwa akiendesha matatu iliyosababisha kifo cha mvulana wa miaka 17 amevunja kimya chake.
Hii ni baada ya makanga wa matatu hio kudaiwa kumsukuma mvulana kutoka kwenye matatu iliyokuwa ikisonga na kukanyagwa na matatu hiyo hadi kufa.
Dereva huyo anayetambulika kwa jina la Geoffrey alisema hafahamu ni nini kilichofanyika ndani ya basi hilo.
"Niliwabeba watu kutoka Pipeline baada ya basi hilo kujaa na tulikuwa tunaelekea mjini, tulipofika karibu na Kware, kondakta alinipa ishara nisimame ili kuruhusu abiria kushuka," Geoffery alisema.
"Katika harakati za kubadili leni ili kuwashusha watu, nilihisi kama nimekanyaga kitu kama jiwe. Nilipoangalia kioo cha pembeni, nikaona ni mtu.” aliongeza Geoffery.
Kisa hicho cha Jumatano kilisababisha msongamano katika barabara ya Outering baada ya umati wenye hasira kuteketeza matatu.
Mwenyekiti wa Embassava Sacco Benson Njoroge ametoa pole kwa familia kwa kufiwa.
Alisema kondakta hakumsukuma kijana huyo kwa sababu mlango wa matatu ulikuwa umefungwa.
“Tumefuatilia suala hilo na sisi kama Sacco, tunasikitika sana kwa kilichotokea, nilizungumza na kaka ya marehemu akaniambia kuwa kaka yake alikua amesahau simu yake na akiwa katika harakati za kutafakari kama ataende kutafuta simu huku akizozana na kondakta lakini mlango ulikuwa umefungwa,” alisema.