Mwanamume apatikana ameuawa Mlolongo kaunti ya Machakos

Alisema mwili huo ulikuwa na majeraha yanayoonekana.

Muhtasari
  • Maafisa wa upelelezi wa DCI kutoka kituo cha polisi cha Mlolongo wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Crime Scene
Image: HISANI

Mwanamume mmoja amepatikana ameuawa  Mlolongo, kaunti ya Machakos.

Mwili wa mwanamume huyo mwenye umri wa kati ya miaka 25 na 30, ulipatikana ukiwa karibu na kanisa la ABC kando ya barabara ya Makanisa ndani ya Kitongoji cha Mlolongo huko Athi River Mashariki siku ya Ijumaa.

Mwanamume huyo anashukiwa kuuawa kwa muda usiojulikana Alhamisi usiku.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Athi River Mashariki Anderson Njagi alisema eneo la tukio lilikuwa limeshughulikiwa na mwili huo kuhamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

"Marehemu ni mtu anayejulikana sana, mkulima huko Lukenya," Njagi aliambia Radiojambo kwenye simu.

Alisema mwili huo ulikuwa na majeraha yanayoonekana.

Kulingana na duru za habari ni kuwa marehemu alitambuliwa na mmoja wa ndugu zake.

Kesi hiyo iliripotiwa katika kituo cha polisi cha Mlolongo kama ripoti ya tukio la kifo cha Mei 19.

Mwili wa marehemu ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Machakos Level 5 ukisubiri kufanyiwa uchunguzi.

Maafisa wa upelelezi wa DCI kutoka kituo cha polisi cha Mlolongo wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.