Maafisa wa DCI kujibu mashtaka ya utekaji nyara katika kesi ya raia wa India waliotoweka

Muhtasari

• Maafisa zaidi kutoka mashirika mengine ya usalama wana uwezekano wa kushtakiwa pamoja na maafisa wa SSU baadaye mwezi huu.

Mifupa inayokisiwa kuwa ya wataalamu wa IT kutoka India na dereva wao yapatikana
Mifupa inayokisiwa kuwa ya wataalamu wa IT kutoka India na dereva wao yapatikana
Image: Maktaba

Idara ya Mashtaka ya Umma (DPP) imeidhinisha mashtaka ya utekaji nyara na kula njama ya kutenda kosa dhidi ya maafisa wa Kitengo cha Utumishi Maalum (SSU) wanaotuhumiwa kuwateka nyara na kuwaua Wahindi wawili waliokuwa wakifanya kazi katika chama cha UDA na dereva wao wa teksi Mkenya.

Kwa mujibu wa gazeti la Nation, Wageni hao wawili, Mohamed Ziad Sami Kidwai na Zulfiqar Ahmed Khan, inasemekana waliwasili nchini Aprili 2022 kujiunga na timu ya Rais William Ruto ya kidijitali ya kampeni, lakini walitoweka Julai 25 baada ya wao na dereva wao wa teksi Nicodemus Mwania kutekwa nyara na watu wasiojulikana nje ya Hoteli ya Ole Sereni jijini Nairobi.

Katika barua kwa mkurugenzi wa Kitengo cha Mambo ya Ndani (IAU), shirika linalochunguza kesi hiyo, Mkurugenzi Msaidizi Mwandamizi wa Mashtaka Joseph Riungu anasema mashtaka yameidhinishwa kusubiri matokeo ya sampuli za DNA ili kubaini iwapo maafisa hao watafunguliwa mashtaka ya mauaji pia.

Mwezi uliopita, wapelelezi watatu wa IAU walisafiri kwenda India, wakiandamana na daktari, kuchukua sampuli za DNA kutoka kwa familia za wahasiriwa. Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, DPP alirejesha jalada la kesi hiyo kwa mara ya nne wiki iliyopita ili kujiridhisha kuwa wapelelezi walitekeleza maagizo ikiwamo kupata sampuli za DNA.

Hati za kiapo zilizowasilishwa katika Mahakama ya Kahawa na mawasiliano kati ya IAU na Huduma ya Wanyamapori ya Kenya yanaonyesha kuwa maafisa zaidi kutoka mashirika mengine ya usalama wana uwezekano wa kushtakiwa pamoja na maafisa wa SSU baadaye mwezi huu.

Mwaka jana, familia za Wahindi hao wawili zilihusisha kutoweka kwao na maajenti wa serikali wakati picha za CCTV zilionyesha gari lao likiwa limezuiwa na kuchukuliwa na watu waliokuwa na silaha ambao waliacha gari kwenye eneo la utekaji nyara.