Daktari apigwa kalamu baada ya kumuomba msafishaji amsaidie katika upasuaji

Upasuaji huo ulifanikiwa kwa bahati nzuri na hakukutokea matatizo yoyote kwa mgonjwa.

Muhtasari

•Daktari huyo alifutwa baada ya kugundulika alitafuta usaidizi wa msafishaji katika upasuaji wa kukata kidole cha mguu wa mgonjwa.

•"Hii haikupaswa kutokea kamwe," Pfeiffer alinukuliwa akisema.

Wataalam wa upasuaji katika chumba cha upasuaji wakimshughulikia mgonjwa
Wataalam wa upasuaji katika chumba cha upasuaji wakimshughulikia mgonjwa
Image: MAKTABA

Hospitali ya Chuo Kikuu cha Mainz, Ujerumani Magharibi ilimfukuza kazi daktari wa upasuaji siku chache zilizopita baada ya kugundulika kwamba alitafuta usaidizi wa msafishaji katika upasuaji wa kukata kidole cha mguu wa mgonjwa.

Wasimamizi wa hospitali hiyo, katika taarifa walieleza masikitiko yao juu ya tukio hilo na kuthibitisha kwamba tangu wakati huo imesitisha uhusiano na daktari wa upasuaji aliyehusika.

Kulingana na chombo cha habari cha SWR, tukio hilo ambalo lilitokea mwaka wa 2020 lilifanikiwa kwa bahati nzuri na hakuna matatizo yoyote yaliyotokea kwa mgonjwa.

Mtendaji mkuu wa hospitali hiyo, Norbert Pfeiffer, alisema daktari huyo wa upasuaji aliamua kimakosa kuendelea na upasuaji huo ingawa hakuna msaidizi aliyehitimu ambaye alikuwepo.

"Hii haikupaswa kutokea kamwe," Pfeiffer alinukuliwa akisema.

Ripoti kutoka Ujerumani zinaonyesha kwamba mgonjwa huyo, ambaye alikuwa amepokea dawa ya ganzi, alipokosa utulivu, daktari alimwomba msafishaji mmoja aliyekuwa karibu naye na ambaye hana uzoefu wa matibabu amshike mguu na ampitishie vifaa vya upasuaji.

Inaripotiwa kuwa kisa hicho kilikuja kujulikana baada ya meneja wa hospitali kuona mavazi ya msafishaji huyo yenye damu mkononi kwenye chumba cha upasuaji.