Kakake Pasta Ezekiel Odero afungua kanisa lake Kisii

Bw Gillack Odero ndiye kasisi mkuu wa Kanisa la New Life Church ambalo linakua kwa kasi katika eneo bunge la Bonchari na waumini kutoka kaunti jirani za Migori na Homa Bay wamejaa pale.

Muhtasari

• Kanisa la Kisii lilianzishwa mwaka mmoja na nusu uliopita, linapatikana Itibo-Rianabaro, karibu na mji wa Suneka.

Mchungaji Ezekiel Odero wakati wa ibada ya Meza ya Bwana Jumamosi.
Mchungaji Ezekiel Odero wakati wa ibada ya Meza ya Bwana Jumamosi.
Image: MAKTABA

Nduguye mdogo wa mhubiri mwenye utata Ezekiel Odero wa Kanisa la New Life Church and Prayer Centre anaendesha tawi la kanisa hilo katika Kaunti ya Kisii katika kile kinachoonekana kuwa biashara ya familia katika uinjilisti, jarida la Nation limefichua.

Bw Gillack Odero, mzaliwa wa nne katika familia ya Odero, ndiye kasisi mkuu wa Kanisa la New Life Church ambalo linakua kwa kasi katika eneo bunge la Bonchari, huku wafuasi kutoka kaunti jirani za Homa Bay na Migori pia wakimiminika kwa ibada zake Jumapili.

Mchungaji Ezekiel, mwanzilishi wa Kanisa la New Life Church and Prayer Centre, anakabiliwa na mzozo wa kisheria unaotokana na shughuli za kanisa hilo lenye makao yake makuu katika Kaunti ya Kilifi, eneo la Mavueni.

Haya yanajiri baada ya Mhubiri Paul Mackenzie wa kanisa la Good News International, pia katika kaunti ya Kilifi, kukamatwa kwa kuwataka wafuasi wake kufunga hadi kufa ili kukutana na Yesu.

Kufikia sasa, miili 240 imetolewa katika ardhi kubwa ya Mackenzie katika kijiji cha Shakahola, huku makumi ya wafuasi wake wakiokolewa wakiwa hai kutoka msituni karibu na nyumba yake ambapo wamekuwa wakifunga.

Mchungaji Ezekiel alikamatwa kuhusiana na vifo vya makumi ya waumini wake katika kanisa lake kuu, ambalo linakusanya maelfu ya watu kutoka kote nchini.

Pia anachunguzwa kuhusiana na uhusiano wake na Mackenzie.

Kanisa la Kisii lilianzishwa mwaka mmoja na nusu uliopita, linapatikana Itibo-Rianabaro, karibu na mji wa Suneka.