Waliookolewa kutoka Shakahola wakataa kula, mmoja afariki kwa njaa

“Tumefanikiwa kuwaokoa watu 91 mpaka sasa japokuwa huyo mmoja amefariki na kuweza kuwakamata watuhumiwa 34 kufikia sasa,” - CS Kindiki.

Muhtasari

• Kindiki alisisitiza kwamba Ni zoezi pekee la kutafuta makaburi na kuwafukua wahanga wa Mauaji ya Shakahola ndio limesitishwa.

• “Utafutaji na uokoaji wa manusura ndani ya Msitu wa Shakahola na Ranchi ya Chakama kwa ujumla utaendelea bila kukatizwa" - Kindiki.

Kindiki atoa takwimu mpya kutoka Shakahola, mmoja wa waliookolewa akifariki kwa kukataa kula.
Kindiki atoa takwimu mpya kutoka Shakahola, mmoja wa waliookolewa akifariki kwa kukataa kula.
Image: Twitter

Waziri wa usalama wa ndani profesa Kithure Kindiki mapema Alhamisi alifika katka kaunti ya Kilifi kushuhudia awamu ya pili ya upasuaji wa miili ambayo imekuwa ikifukuliwa kutoka makaburi ya shamba la Shakahola lenye upana wa ekari 800.

Akizungumza na wanahabari, Kindiki alifichua kwamba hata baada ya waumini wengine wa kanisa lenye mafunzo potovu la mchungaji Paul Mackenzie kuokolewa wakiwa hai, wengi wao wamekuwa wakisusia kula na tayari mmoja wao amefariki kutokana na njaa.

“Jana pia tulipoteza mtu mmoja miongoni mwa watu ambao waliokolewa kutoka shamba hilo na kupelekwa hospitalini kwa ustawi, kwa sababu waliendelea kukataa chakula. Tulijaribu kadri ya uwezo wetu kuwalazimisha kula lakini walikataa na kugoma kabisa na kujumuisha mgomo wao na unyonge waliokuwa nao, mmoja aliweza kufa,” Kindiki alisema.

Waziri huyo alifichua kwamba mpaka sasa idadi ya maiti ambazo zimefukuliwa kutoka shamba hilo la Shakahola inaelekea mia mbili hamsini huku pia akisema shughuli ya upasuaji wa miili iliyofukuliwa katika awamu ya pili ulifanyika na majibu yake yatatolewa baadae.

“Miili ambayo tumeshafukua kutoka msitu wa Shakahola mpaka sasa imefikia 241, na hiyo inajumuisha mizoga mitano ya watu ambayo ilipatikana na maafisa wetu katika siku mbili tofauti na inatarajiwa kufanyiwa uchunguzi na mwanapatholojia,” alisema.

“Tumefanikiwa kuwaokoa watu 91 mpaka sasa japokuwa huyo mmoja amefariki, tumefanikiwa pia kuchukua sampuli za DNA kutoka kwa visa 93, tumewakutanisha manusura 19 na familia zao na kuweza kuwakamata watuhumiwa 34 kufikia sasa,” Kindiki alitoa takwimu.

Kindiki alisisitiza kwamba Ni zoezi pekee la kutafuta makaburi na kuwafukua wahanga wa Mauaji ya Shakahola ndio limesitishwa ili kutoa nafasi ya kuandaa utaratibu wa uchunguzi wa baada ya kifo cha miili 123 ya ziada iliyopatikana katika Awamu ya 2 ya zoezi la ufukuaji.

“Utafutaji na uokoaji wa manusura ndani ya Msitu wa Shakahola na Ranchi ya Chakama kwa ujumla utaendelea bila kukatizwa na utapanuliwa hadi kwenye kingo za Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo Mashariki katika siku zijazo kwa kutumia utafutaji wa ardhini na ndege zisizo na rubani,” Waziri alisema.