Rais Dkt. William Ruto amekiri kwamba lazima kila mtu nchini atoe ushuru licha ya hali yake au tabaka.
Amelizungumzia hili alipokuwa katika jumba la kukusanyia ushuru la Times Tower jijini Nairobi Mei 26 huku zikiwa zimesalia siku chache kwa KRA kufunga shughuli hiyo.
Katika hotuba yake Ruto alisema, “ Ni wajibu wa kila Mkenya kutoa ushuru ndipo kuwezesha taifa kusonga mbele na liangazie miundo mbinu kwa watu.” Haya yanajiri huku naibu wa Rais Rigathi Gachagua aliyeandamana naye katika jumba hilo akisema kuwa, njia pekee ya taifa kusonga mbele si kwa kuomba bali ni serikali yenyewe kujitafutia njia ya kupata hela.
“Njia pekee ya kuendeleza nchi mbele si kwa kuomba bali ni kutafuta mjia inayoweza kusaidia kujipatia hela hasa kupitia maliasili yetu na kwa kutafuta ushuru kwa kila mwananchi.” Gachagua alisema. aliendelea na kusema kuwa pesa zinaombwa ni deni na hivyo lazima siku moja litalipwa.
Kwa upande wake Rais, alitilia mkazo kwa maafisa wa KRA ambapo alisema kwamba barabara, hospitali shule na hali nzuri katika mawasiliano zimefanikishwa kwa sababu ya ushuru unaotoka kwa wananchi. Ruto aliendelea kwa kusema kuwa, jamii huangaziwa kwa kiwango cha elimu ,barabara,hospitali na mengine muhimu wala si kwa watu wanaojimudu katika jamii hiyo.
“Licha ya kuwa ushuru ni wa lazima na si wa kuhepukika,lazima pia serikali ishike doria ndipo kuhakikisha kwamba kuna uwazi na uwajibikaji kwa kila afisaa anayeshughulikia maswala ya ushuru.” Ruto aliendelea kwa kulinganisha kiwango cha ushuru nchini na baadhi ya mataifa ya Afrika hasa Morocco ambao kiwango chao cha ushuru kipo juu.
Rais alisema pia hataruhusu ufisadi ulemaze taifa,waaidha atakuwa katika mstari wa mbele kuyaziba mashimo yote ambayo yanajaribu kuzivuja pesa za mwananchi.