Migori: Watu 5 wauawa kwa risasi huku waombolezaji wakivamia kituo cha polisi

Waombolezaji hao waliandamana kwa fujo kuelekea kituo cha polisi wakiwa wamebeba mwili wa mtu aliyeuawa na wezi, walikuwa na gari lililosheheni mawe, viberiti na panga.

Muhtasari

• Kulingana na ripoti ya polisi, watu hao wenye ghasia wakiwa na silaha chafu waliwavamia maafisa wa polisi waliokuwa wakilinda lango.

• Jitihada zao za kuteketeza kituo hicho na kuwaachilia washukiwa waliokuwa chini ya ulinzi wa polisi ndizo zilisababisha maafisa hao kufyatua risasi.

Waombolezaji 5 vwauawa kwa risasi na polisi katika maandamano kituoni Isebania.
Waombolezaji 5 vwauawa kwa risasi na polisi katika maandamano kituoni Isebania.
Image: Twitter

Maandamano ya kupinga ukosefu wa usalama Kuria Magharibi, Kaunti ya Migori yaligeuka kuwa mbaya baada ya watu watano kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Watano hao walikuwa miongoni mwa makumi ya Waombolezaji waliokuwa wamebeba mwili wa mfanyabiashara aliyeuawa na majambazi wiki moja iliyopita.

Wakiwa na jeneza na sauti za kuomboleza, walivamia Kituo cha Polisi cha Isebania, Kaunti ya Migori ambapo waliwavamia maafisa hao wa polisi.

Kulingana na ripoti ya polisi, watu hao wenye ghasia wakiwa na silaha chafu waliwavamia maafisa wa polisi waliokuwa wakilinda lango.

Jitihada zao za kuteketeza kituo hicho na kuwaachilia washukiwa waliokuwa chini ya ulinzi wa polisi ndizo zilisababisha maafisa hao kufyatua risasi, KBC waliripoti.

“Kikundi cha wafanya ghasia waliokuwa wakiusindikiza mwili wa mwanaume mmoja kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mtakatifu Akidiva Mindira Mabera walivamia kituo hicho wakiwa kwenye gari la mizigo lililojaa mawe, kiberiti na panga. Walivunja madirisha ya ghala la silaha, ofisi ya OCS na ofisi zingine kwa mawe. Walianza kuharibu mageti ya seli wakitaka wote walioko kizuizini waachiliwe” inasomeka ripoti hiyo kwa sehemu kulingana na KBC.

Polisi wanasema shambulio hilo lilipangwa.

“Baada ya kuwatimua maafisa wanaosimamia ofisi ya ripoti, hifadhi ya silaha na seli, jambo hilo liliwafanya maafisa hao kutetea uokoaji wa nguvu wa wafungwa waliokuwa kizuizini na wizi wa bunduki kwa kutumia risasi za moto. Kwa bahati mbaya, hii ilisababisha vifo vya watu wanne wasiojulikana,” ripoti hiyo inasema.

OCPD wa Kuria Magharibi Cleti Kimayio alithibitisha kisa hicho na kuongeza miili hiyo imehamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mtakatifu Akidiva Mindira Mabera.

Afisa mmoja wa polisi anauguza majeraha.