Chama cha wamiliki wa matatu nchini (MOA) kimetangaza kuwa kitaongeza nauli za mabasi kwa angalau asilimia 30 kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta.
Mnamo Jumanne, mwenyekiti wa MOA Albert Karakacha alipokuwa akihutubia wanahabari alisema marekebisho hayo yatawasaidia wawekezaji katika sekta ya uchukuzi kuweza kufaidika kutoka kwa biashara zao.
"Kumekuwa na ongezeko kubwa la bei ya mafuta na matumizi mengine... Tulishauriana kabla ya kufika katika ongezeko la asilimia 30," alisema.
Kulingana na Karkacha, bei za vipuri vya gari na matairi pia zimepanda kwa kiwango kikubwa na hii ilichangia kuongezeka kwa bei ya nauli.
Abiria wanaosafiri kutoka sehemu mbali mbali za mji wa Nairobi hadi CBD watalipa shilingi 10 au shilingi 20 za ziada katika mabadiliko hayo mapya.
Abiria wa Kajiado, Machakos, Muranga na Kiambu watatozwa shilingi 20 hadi shilingi 50 za ziada ili kusafiri hadi mijini.
Kutoka Mombasa CBD hadi miji mingine kama vile Voi, Malindi, Ukunda, Kilifi, Lamu, Tana River, Wundanyi na Mwatate abiria watatumia shilingi 30 hadi shilingi 70 za ziada kwenye nauli ya matatu.
Nauli za matatu kutoka eneo la Nyanza hadi Nairobi na kurudi zitaongeza nauli kwa shilingi 100 hadi shilingi 200. Kwa huduma ya mjini, abiria watalipa shilingi 10 hadi shilingi 20 za ziada.
Magari yanayoelekea Nairobi kutoka Kitale, Bomet, Kericho, Narok, Kapenguria, Baringo, Eldoret, Nakuru, Kapsabet, na Naivasha yatatoza shilingi 100 za ziada hadi shilingi 200.
Mnamo Juni 30, EPRA iliongeza bei ya mafuta huku bei ya mafuta ya petroli ikipanda kwa shilingi 13.49, Dizeli shilingi 12.39 na mafuta ya taa kwa shilingi 11.96 jijini Nairobi.
Ongezeko hilo ni matokeo ya sheria ya fedha ya 2023 ambayo inaongeza VAT kwenye mafuta kuwa asilimia 16 kutoka asilimia 8.
"Kwa mujibu wa Sheria ya Fedha, 2023, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye Super Petrol (PMS), Dizeli (AGO) na Mafuta ya Taa (IK) imefanyiwa marekebisho kutoka asilimia 8 hadi 16 kuanzia tarehe 1 Julai 2023," EPRA ilisema.