Maafisa watano walijeruhiwa wakati wa maandamano ya Saba Saba - polisi

Maafisa hao walijeruhiwa wakati wa maandamano ulioandaliwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Muhtasari

• Waandalizi wa maandamano hayo wamesisitiza kuwa ni polisi waliochochea hali hiyo kuwa ya vurugu.

• Wakati wa tukio hilo magari mawili ya polisi- Toyota Land cruiser na Ranger- yalivunjwa vioo vyao vya mbele.

wakati wa ibada ya kanisa huko Tharaka Nithi mnamo Mei 21, 2023.
Waziri wa usalama wa ndani Kindiki Kithure wakati wa ibada ya kanisa huko Tharaka Nithi mnamo Mei 21, 2023.
Image: HISANI

Polisi wanasema takriban maafisa watano walijeruhiwa katika maandamano ya saba saba siku Ijumaa jijini Nairobi.

Polisi waliwapiga risasi na kuwaua watu sita waliokuwa wakiandamana katika maeneo ya Kisii, Migori na Kisumu.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alithibitisha polisi kuwapiga risasi na kuwaua watu sita katika maandamano hayo.

"Ijumaa iliyopita, wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na muungano wa Azimio, watu sita waliuawa na wengine kujeruhiwa, wakiwemo maafisa wa usalama. Uhuru wa kujumuika na haki ya kuandamana/kunyang’anya mali haijumuishi haki ya kusababisha ghasia na kupora mali.” Waziri Kindiki alisema.

"Siku ya Jumatano, mtu yeyote anayetishia kufanya nchi isitawalike kupitia ghasia, uporaji, machafuko na umwagaji damu atashughulikiwa vilivyo, kwa mujibu wa sheria," alisema.

Waandalizi wa maandamano hayo wamesisitiza kuwa ni polisi waliochochea hali hiyo kuwa ya vurugu.

Maandamano hayo yaliitishwa kuadimisha siku ya Saba Saba, ambayo inahusishwa na mapambano ya nchi hiyo ya mfumo wa vyama vingi.

Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi(IPOA) inasema inachunguza visa vya ufyatuaji risasi na polisi kwa waandamanaji ambavyo viliripotiwa.

Zaidi ya watu 100 walikamatwa katika maandamano ya nchi nzima. Baadaye mahakama iliwaachilia.

Maafisa hao walijeruhiwa katika eneo la Kamkunji wakati waandamanaji wakipambana na polisi.

Wakati wa tukio hilo magari mawili ya polisi- Toyota Land cruiser na Ranger- yalivunjwa vioo vyao vya mbele.

Maafisa waliojeruhiwa walitibiwa hospitalini na kuruhusiwa.