Katibu mkuu wa chama cha ODM, Edwin Sifuna sasa anamtaka seneta wa Nandi Samson Cherargei kukabiliana naye na kuachana na waandamanaji watimize uhuru wao wa kikatiba wa kuandamana.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari nchini, Sifuna alimwagiza seneta huyo mwenzake kuelekeza nguvu zake kupigana masumbwi naye kuliko kuangazia kuwatafuta vijana ili kuzua vurugu wakati wa maandamano yanayoongozwa na upande wa Azimio.
“Mtu kama Cherargei mkiangalia anaeza piga nani hapa, Anaongea sana kwa sababu anajua atajificha katika mbawa za vitengo vya usalama nchini. Seneta Cherargei kabla ya kupanga vijana kupigana na wandamanaji we kuja tu tupatane tupigane tu watu wawili.”
Sifuna alidai kuwa tuvuti ya muungano ya Azimio ya kukusanya saini za kumuondoa Rais Ruto mamlakani imejaribiwa kudukuliwa zaidi ya mara 1000 bila mafanikio.
“Ya mwisho, wamekuwa wakilia ati mpango wa kukusanya saini milioni 10 haiendi mahali popote. Lakini watu hawa hawa wanang’ang’ana kudakua tovuti wa kukusanya saini. Tumepokea zaidi ya mashambulizi 1000 katika tuvuti yetu.”
Sifuna aliongeza kuwa mpango wao wa kuandamana siku tatu ndani ya wiki moja kuanzia siku ya Jumatano hadi Ijumaa utaendelea hadi pale viongozi serikalini watakapoisikia kilio cha Wakenya wa kushuka kwa bei ya juu ya gharama.
“Tunasema Wakenya wanataka kukula, na wanataka kukula leo hii na haijalishi ni muda mgani mtaendelea kufunika msaskio yen. Tutapiga hiyo maskio kofi mpaka ifunguke mskie kilio cha Wakenya.”
Viongozi katika muungano tawala wa Kenya Kwanza wameendelea kujipiga kifua wakiwaonya upande wa Azimio dhidi ya kufanya maandamano.
Waziri wa usalama wa Ndani Kithure Kindiki, siku ya Jumatano akizungumza akiwa eneo la Sondu aliwafananisha waandamanaji wenye jeuri ya Upinzani na magaidi.
Kindiiki alisema waandamanaji ambao wamekuwa wakijihusisha na uharibifu wa mali katika maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali hawana tofauti na magaidi.
“Tumekuwa tukipambana na Al Shabaab na majambazi katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya lakini sasa sisi kundi jingine la wahalifu ambao wako katika siasa. Wote wako kwenye kundi moja la Whatsapp,” alisema.
Sasa ni kuwapa viongozi hawa jicho tu na kusubiri kuona kile kitakachotokea siku ya Jumatano. Letu ni kukutakia wewe mpenzi msikilizaji usalie salama na mwenye afya.