Afisa mkuu wa kaunti ya Kilifi auawa na kijakazi wake

Karisa alikuwa mwanaharakati aliyejitolea na aliyependa usimamizi wa mazingira.

Muhtasari
  • Kamanda wa polisi kaunti ya Kilifi Fatuma Hadi alithibitisha kisa hicho, akisema polisi wataanza uchunguzi kuhusu kisa hicho na msako wa kumtafuta msaidizi wa nyumba.

Afisa Mkuu wa Madini na Uchumi katika Kaunti ya Kilifi, Rahab Karisa, ameuawa katika mazingira ya kutatanisha.

Kulingana na mlinzi wa nyumba ya Karisa iliyoko eneo la Mnarani, afisa huyo wa serikali ya kaunti aliuawa kwa kudungwa kisu na usaidizi wa nyumba yake kabla ya kutoroka.

Afisa Mkuu huyo aliripotiwa kurejea nchini Jumatano kutoka kwa safari ya kikazi nchini Italia.

Kamanda wa polisi kaunti ya Kilifi Fatuma Hadi alithibitisha kisa hicho, akisema polisi wataanza uchunguzi kuhusu kisa hicho na msako wa kumtafuta msaidizi wa nyumba.

Kulitokea ugomvi kati yake na mhudumu wa nyumba, ambaye alitoweka kabla ya maafisa wa kampuni ya kibinafsi kufika kwa kazi zao za asubuhi.

Taarifa zinadai kuwa mwili wa Afisa Mkuu huyo ulikutwa ukiwa umelala kifudifudi kwenye dimbwi la damu chumbani kwake na nyaraka zikiwa zimetapakaa kitandani na sakafuni.

Mwili wa marehemu ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya kaunti ya Kilifi ukisubiri kufanyiwa uchunguzi.

Karisa alikuwa mwanaharakati aliyejitolea na aliyependa usimamizi wa mazingira.

Hadi kifo chake, alikuwa akihudumu kama Afisa Mkuu wa Kaunti katika utawala ulioongozwa na Gavana Gideon Mung'aro.

Alihusika katika miradi ya kuhifadhi mazingira katika Kaunti ya Kilifi akifanya kazi kwa karibu na jamii na kusukuma mbinu bora za kimataifa kuelekea uendelevu.

Kabla ya hapo, Karisa alikuwa ametumia umahiri wake kama mshauri wa utendakazi wa mazingira na kijamii katika shirika la reli la Kenya kabla ya kujiunga na Mamlaka ya Barabara za Vijijini Kenya kama mwanamazingira kwa miaka 2.