Mwaka 1 wa Ruto ofisini: Kindiki mtumishi bora wa umma Gachagua akishika mkia - ripoti

Hata hivyo, utafiti huo uliofanyika katika maeneo 8 ya kikanda Kenya ilibaini kwamba asilimia 53 ya Wakenya wanahisi taifa linaelekea pabaya.

Muhtasari

• Kindiki alipata asilimia ya 56% kwa utendakazi wake akifuatwa na waziri wa elimu Ezekiel Machogu kwa asilimia ya 55%.

• Katika utafiti huo, naibu wa rais Rigathi Gachagua alitajwa na wengi kama mtumishi wa umma katika serikali ya Ruto ambaye hajafanya kikubwa cha mno.

Gachagua na Kindiki
Gachagua na Kindiki
Image: Facebook

Jumatano Septemba 13 iliadhimisha mwaka mmoja tangu rais Ruto alipoapishwa rasmi katika uwanja wa Kasarani kuchukua hatamu kama rais wa Tano wa Kenya.

Kufuatia kuadhimisha mwaka mmoja, kampuni ya utafiti ya Infotrak ilifanya utafiki mwezi uliopita ili kutathmini jinsi serikali hiyo imekuwa ikifaulu katika sekta mbali mbali lakini pia kwa kiasi kipi ambacho serikali ya Kenya Kwanza imefanikiwa kutimiza na kutelekeza yale waliyoyaahidi kwa wnanchi wakati wa kampeni katika manifesto yao.

Infotrak waliangazia utendakazi wa baraza la mawaziri wa Ruto ambapo Wakenya wengi walihisi kwamba rais Ruto mwenyewe amejaribu kadri ya uwezo wake kufanya kazi na hivyo akapewa alama ya C kwa asilimia 55% ya ufanisi wa manifesto yake.

Katika utafiti huo, naibu wa rais Rigathi Gachagua alitajwa na wengi kama mtumishi wa umma katika serikali ya Ruto ambaye hajafanya kikubwa cha mno na hivyo kupewa alama ya D.

Kwa upande wa mawaziri, waziri wa usalama wa ndani Profesa Kithure Kindiki alishikilia nafasi ya kwanza kama waziri aliyefanya kazi kwa juhudi kubwa huku mwenzake wa kawi Davis Chirchir alipigiwa kura kama waziri aliyefeli pakubwa katika majukumu yake.

Kindiki alipata asilimia ya 56% kwa utendakazi wake akifuatwa na waziri wa elimu Ezekiel Machogu kwa asilimia ya 55%, wizara ya kilimo yake Mithika Linturi ikiwa ya tatu kwa asilimia 54 na wizara ya barabaraba ikiongozwa na wakili Kipchumba Murkomen ikifunga asilimia 50 kwenda juu kwa kupata 54%.

Wizara ya biashara na viwanda yake Moses Kuria ilipata asilimia 47, ile ya Leba yake Florence Bore ikiwa na asilimia 46, ya fedha ikiwa na asilimia 44 na ile ya kawi yake Chirchir ikifunga kwa asilimia 43.

Hata hivyo, utafiti huo uliofanyika katika maeneo 8 ya kikanda Kenya ilibaini kwamba asilimia 53 ya Wakenya wanahisi taifa linaelekea pabaya.