Jamaa atiwa mbaroni kwa kuchafulia DP Gachagua jina Twitter

Mtumizi huyo wa Twitter anayetumia jina la utambulisho la WanjikuHSC alitambulika kuwa ni mwanamume kwa jina halisi la Silvance Abeta.

Muhtasari

• Alikamatwa Ijumaa katika kile wapelelezi wanasema ni kueneza propaganda dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na vigogo wengine wa serikali na mashirika.

Mwanaume aliyekamatwa
Mwanaume aliyekamatwa
Image: Sagwe

Mtumizi mmoja wa mtandao wa X, awali ukijulikana kama Twiter amejipata pabaya baada ya kutoa matamshi yasiyo ya kweli dhidi ya naibu wa rais Rigathi Gachagua.

Mtumizi huyo aliyetambulika kwa jina Silvance Adongo Abeta ambaye anatumia akaunti ghushi yenye jina la utambulisha la mwanamke – Wanjiku HSC – alikuwa ametoa matamshi yasiyo ya kweli kwamba naibu wa rais Rigathi Gachagua alikuwa anaandaa njama ya kumdhuru mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

 Alikamatwa Ijumaa katika kile wapelelezi wanasema ni kueneza propaganda dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na vigogo wengine wa serikali na mashirika.

Kwa mujibu wa Citizen, Hati ya mashtaka ya Abeta inaonyesha kuwa anashitakiwa kwa makosa ya mtandaoni, miongoni mwao yakiwemo ya unyanyasaji mtandaoni na kueneza habari potofu.

"Mshtakiwa ni mnyanyasaji wa mtandaoni anayetumia akaunti ya Twitter (X) ya mbishi inayojulikana kama @WanjikuHSC kwa jina Karen Wanjiku HSC. Ili kuficha utambulisho wake wa kweli, mlalamikiwa anatumia akaunti hiyo ya mbishi kuchapisha habari za uwongo, uonevu na mtandao kuwanyanyasa Mkenya asiye na hatia. wananchi," karatasi ya mashtaka ilisomeka kama ilivyonukuliwa na Citizen.

Kukamatwa kwake kulikuja baada ya kutoa chapisho tata lililowagusa DP Rigathi Gachagua na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Abeta sasa anachangisha fedha akiomba watu wema kumsaidia kulipa dhamana yake.

Kulingana na orodha aliyoshiriki mtandaoni, miongoni mwa wanaodaiwa kuchangia kuachiliwa kwake ni Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ambaye alitoa Ksh 15,000.