Bomet: Nyuki wavamia boma na kumuua mtoto wa miaka 2

Mtoto huyo alikimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Sigor katika jaribio la kuokoa maisha yake - lakini kwa bahati mbaya alitangazwa kuwa amefariki alipofika.

Muhtasari

• Wanafamilia wengine walitibiwa na kuruhusiwa.

• Kulingana na Mutai, nyuki hao walizunguka boma hilo kwa saa nyingi - na kuwalazimu majirani kujifungia ndani ya nyumba zao kwa hofu ya kushambuliwa.

Nyuki
Nyuki
Image: University of Melbourne

Mtoto wa miaka miwili ameripotiwa kufariki baada ya kushambuliwa na bumba la nyuki alipokuwa akicheza nje ya boma lao katika eneo la Chepkosa kaunti ya Bomet.

Kwa mujibu wa taarifa, Wanafamilia wengine watano waliachwa wakiuguza majeraha mabaya kufuatia shambulio hilo.

Afisa wa usimamizi wa majanga kaunti ya Bomet Stanley Mutai alithibitisha kisa hicho.

"Mtoto huyo alikuwa akicheza nje ya nyumba yao wakati nyuki ghafla walianza kuzungukazunguka kwenye boma - na kuanza kumuuma kila mtu aliyekuwa nje," alisema Mutai.

Mtoto huyo alikimbizwa katika hospitali ya kaunti ndogo ya Sigor katika jaribio la kuokoa maisha yake - lakini kwa bahati mbaya alitangazwa kuwa amefariki alipofika.

Wanafamilia wengine walitibiwa na kuruhusiwa.

Kulingana na Mutai, nyuki hao walizunguka boma hilo kwa saa nyingi - na kuwalazimu majirani kujifungia ndani ya nyumba zao kwa hofu ya kushambuliwa.

Mwili huo ulipelekwa katika chumba cha maiti cha hospitali ya Rufaa ya Longisa.