• Petrol sasa imeongezeka kwa Ksh.16.96, Dizeli inapanda kwa Ksh.21.32, huku Mafuta ya Taa yakipanda juu zaidi kwa Ksh.33.13 kwa lita.
Wakenya watazidi kung’atwa hata Zaidi kutokana na gharama ya juu ya maisha baada ya shirika la kukadiria bei za kawi, EPRA kutangaza bei mpya za bidhaa za kawi – bei ambazo zimeanza kutekelezwa kuanzia usiku wa manane wa kuamkia Septemba 15, kote nchini.
EPRA, katika taarifa kwa vyumba vya habari Alhamisi usiku, ilifichua kuwa bei ya Super Petrol sasa imeongezeka kwa Ksh.16.96, Dizeli inapanda kwa Ksh.21.32, huku Mafuta ya Taa yakipanda juu zaidi kwa Ksh.33.13 kwa lita.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Daniel Kiptoo Bargoria alibainisha kuwa bei iliyoongezeka ilitokana na uzani wa wastani wa gharama ya bidhaa za petroli zilizosafishwa kutoka nje.
“Bei hizo ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani ya 16% (VAT) kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Fedha ya 2023, Sheria ya Kodi (Marekebisho) ya Sheria ya 2020 na viwango vilivyorekebishwa vya Ushuru wa Bidhaa vilivyorekebishwa kwa mfumuko wa bei kwa mujibu wa Notisi ya Kisheria Na. 194 ya 2020," alisema.
Kufuatia tangazo hilo, Petroli sasa imeanza kuuzwa kwa shilingi 211.64 jijini Nairobi kutoka bei ya awali ya shilingi 194.68, na Dizel itauzwa kwa shilingi 200.99 kutoka kwa bei ya mwezi jana ya shilingi 179.67 huku mafuta ya taa yakiongezeka hadi shilingi 202.61 kutoka kwa bei ya mwezi Agosti ya shilingi 169.48 jijini Nairobi.
Viwango kwa lita moja mjini Mombasa vitakuwa, Super Petrol (Ksh.208.58), Dizeli (Ksh.197.93) na Mafuta ya Taa (Ksh.199.54) huku Kisumu; Super Petrol (Ksh.211.40), Dizeli (Ksh.201.16) na Mafuta ya Taa (Ksh.202.77).