Gavana Wavinya Ndeti amsihi Rais Ruto kushughulikia bei ya juu ya mafuta

Kulingana na Gavana wa Machakos, gharama ya mafuta inapopanda, gharama za usafiri huongezeka

Muhtasari
  • Hii ni huku kukiwa na lawama kutoka kwa umma na viongozi sawa dhidi ya kuongezeka kwa gharama ya mafuta ambayo inatishia kuyumba katika sekta mbalimbali za uchumi.
GAVANA WA KAUNTI YA MACHAKOS WAVINYA NDETI
Image: KWA HISANI

Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti amemtaka Rais William Ruto kutafuta suluhu mwafaka ili kuwaepusha Wakenya kutokana na athari mbaya ya kupanda kwa bei ya mafuta.

Hii ni huku kukiwa na lawama kutoka kwa umma na viongozi sawa dhidi ya kuongezeka kwa gharama ya mafuta ambayo inatishia kuyumba katika sekta mbalimbali za uchumi.

Kulingana na Gavana wa Machakos, gharama ya mafuta inapopanda, gharama za usafiri huongezeka hali ambayo hupanda bei ya bidhaa muhimu kama vile chakula na bidhaa nyingine za matumizi, hivyo basi kuwaelemea zaidi kaya za Kenya ambazo tayari zinatatizika kujikimu kimaisha.

"Tutawalishaje watoto hawa? Hatuwezi kukaa kimya kuhusu hilo. Maisha yanazidi kuwa magumu kwa kila mtu," Wavinya alieleza wakati wa hafla ya kanisani Jumamosi.

Gharama ya mafuta nchini Kenya ilifikia rekodi ya juu siku ya Ijumaa ikivuka alama ya Shilingi 200 kwa mara ya kwanza. Hili limeibua kengele kote nchini, hali iliyowafanya wananchi kuhoji ni vipi wataweza kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha.

Jumapili naibu Rais alivunja kimya chake kuhusu bei ya juu ya mafuta huku akisema kwamba imeongezeka ulimwenguni kote na kuwasihi Wakenya wawe wavumilivu.