Polisi wawili wakamatwa kwa madai ya kuitisha rushwa ya elfu 50

Wawili hao, naibu OCS ambaye alikuwa akihudumu kama kaimu OCS wakati huo, na afisa mdogo, walikamatwa Jumatatu jioni.

Muhtasari

• Gari hilo lilikuwa limezuiliwa kwa takriban miezi miwili licha ya mlalamishi kupata na kuwasilisha kwa kaimu OCS amri ya mahakama ya kuachiliwa kwake.

• Kufuatia kukamatwa kwao na kufanyiwa uchuguzi katika Kituo cha Integrity Center, baadaye waliwekwa kizuizini katika kituo cha Kilimani wakisubiri hatua zaidi.

Pingu
Image: polisi wawili washikwa kwa madai ya hongo

Maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi imewakamata maafisa wawili wa polisi katika Kaunti ya Kiambu kwa kudai  hongo ya shilingi 50,000 ili kuachilia gari lililozuiliwa.

Wawili hao, naibu OCS wa kituo cha polisi katika eneo hilo na ambaye alikuwa akihudumu kama OCS wakati huo, na afisa mdogo, walikamatwa Jumatatu jioni.

Gari hilo lilikuwa limezuiliwa kwa takriban miezi miwili licha ya mlalamishi kuwasilisha kwa kaimu OCS agizo la mahakama ili liachiliwe.

Kufuatia kukamatwa kwao na kufanyiwa uchunguzi katika Kituo cha Polisi cha Integrity Centre, baadaye waliwekwa kizuizini katika kituo cha Kilimani wakisubiri hatua zaidi.

EACC ilichukua hatua kufuatia uchunguzi kuhusu madai kwamba mnamo Julai 26, 2023, mlalamishi alikamatwa alipokuwa akisafirisha mitungi ya gesi hadi eneo lake la biashara huko Githunguri.

Mlalamishi alidaiwa kusafirisha mitungi hiyo kwa kutumia gari lisiloruhusiwa, gari la saloon. Maafisa hao waliendelea kumkamata na kumzuilia katika kituo cha polisi.

Siku iliyofuata, alifikishwa katika Mahakama ya Githunguri na kushtakiwa kwa kosa la kusafirisha mitungi ya gesi kwa kutumia gari lisiloidhinishwa.

Mwanamume huyo aliachiliwa kwa bondi ya Sh70,000 na hakimu akakubali ombi lake la kutaka gari hilo lirudishwe kwake. Naibu OCS aliamriwa kuachilia gari hilo mara moja, bila masharti.

  Mlalamishi alipoenda, naibu OCS alidai ada ya lazima ya Sh50,000 kama motisha ya kuachiliwa kwa gari hilo.

Aliomba gari hilo litolewe kwa mujibu wa amri ya mahakama lakini ofisa huyo alikaidi na kuamuru atoke nje ya kituo hadi siku alipopata fedha hizo. Ni wakati huu ambapo mlalamishi aliitaka EACC kuingilia kati na uchunguzi ambao ulibaini yaliyotajwa hapo juu kuanzishwa.

Baada ya kuthibitisha madai hayo, shirika la kupambana na ufisadi lilianzisha operesheni iliyopelekea kukamatwa kwa kaimu OCS na afisa mdogo. Walikamatwa kituoni  baada ya kupokea "ada ya motisha" iliyodaiwa.