Mahakama ya Kilifi imewapa polisi hadi Jumatatu kuwashikilia washukiwa 11 kuhusiana na vifo vya watoto wawili wanaodaiwa kufariki kutokana na mafundisho ya kidini.
Hakimu mkuu wa Kilifi Justus Kituku siku ya Alhamisi aliamua kwamba 11 hao ambao ni pamoja na wazazi wa marehemu wanapaswa kuendelea kuzuiliwa na polisi hadi Jumatatu ambapo polisi wanatarajiwa kutoa ripoti yao.
Kituku alisema ingawa ni haki kwa mujibu wa Ibara ya 49 ya katiba kwa mshtakiwa kupewa bondi, baadhi ya mazingira yanaweza kusababisha mahakama kuwanyima dhamana.
“Mambo kama vile utata wa suala linalochunguzwa, upeo wa upelelezi, uzito wa kosa linalochunguzwa, uhusiano wa watu waliokamatwa na wahasiriwa, na wanaotarajiwa kuwa mashahidi. Katika kisa hiki, kuna madai ya mafundisho ya itikadi kali yaliyosababisha vifo vya watoto, na kama tumejifunza kutoka kwa suala la Shakahola, uchunguzi huu unaweza kuwa mpana," ilisoma sehemu ya uamuzi huo.
Polisi wanaamini kuwa watoto hao wenye umri wa miaka 11 na 13 walifariki baada ya wazazi wao kukosa kuwapeleka hospitalini kutokana na imani ya kanisa lao.
Ni washiriki wa Kanisa la Mungu Neno la Kweli linaloamini katika uponyaji wa kimungu. Waumini wa kanisa hilo hawaamini kwenda hospitalini bali huomba tu wakati mtu anakuwa mgojwa.
Kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Kilifi Kaskazini Kenneth Maina alisema mmoja wa watoto hao alifariki Jumamosi nyumbani kwao. Wa pili alifariki siku ya Jumapili nyumbani kwa muumini wa kanisa hilo.
"Tulipata habari kutoka kwa umma siku ya Jumapili kuhusu kifo kinachoshukiwa cha mtoto mdogo na watu walikuwa wakipanga kuficha kifo hicho'.polisi walisema
Tulifanikiwa kufika mahali walipokuwa wamekusanyika lakini watoto walikuwa wamefukuzwa. Mwili wa mtoto pia ulikuwa umetolewa.
Tuliwakamata wengine na kwenda kwenye boma la wazazi ambapo tuliwakamata wengine. Kufikia wakati huo wazazi walikuwa hawajajua kifo cha mtoto wa pili,” alisema. Maina alisema dini hiyo haina jengo la kimwili ambapo wanafanyia ibada zao bali kila Jumapili hukusanyika katika kiwanja cha mwanachama yeyote atakayejitolea kuwakaribisha.
“Ni changamoto kuwafuatilia kwa sababu hawana kanisa. Kila wakati huduma yao inafanywa katika eneo tofauti ambalo linaweza kuwa hata mji tofauti.
Polisi waliomba kuwazuilia washukiwa hao ili uchunguzi wa maiti ufanyike.