KAMPUNI ya kusambaza umeme nchini Kenya (KPLC) imeonya kuhusu kukatizwa kwa umeme katika maeneo kadhaa nchini siku ya Jumanne.
Katika taarifa ya Jumatatu jioni, kampuni hiyo ilitangaza kuwa baadhi ya maeneo ya kaunti sita nchini Kenya zitakosa umeme kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja jioni. Kaunti zitakazoathirika ni pamoja na kaunti ya Nairobi, Kiambu, Migori, Homa Bay, Embu na kaunti ya Kilifi.
Katika kaunti ya Nairobi, sehemu ya mtaa wa Umoja na Rosslyn itakosa umeme kati ya saa tatu asubuhi na kumi na moja jioni.
Maeneo ya Ting’ang’a, Ngemwa, Sigona na Zambezi katika kaunti ya Kiambu yataathiriwa na kupotea kwa umeme kwa sehemu kubwa ya siku ya Jumanne hadi saa kumi na moja jioni.
Katika kaunti ya Migori, maeneo ya Kakrao na God Jope yatakosa nguvu za umeme kati ya saa tatu asubuhi na tisa alasiri. Wakati uo huo, eneo la Gogo Katuma katika Kaunti ya Homa Bay pia litaathirika.
Sehemu za kaunti ya Embu ikijumuisha Uwanja wa Ndege wa Embu pia zitapoteza nguvu ya umeme kati ya tatu asubuhi na saa kumi na moja jioni.
Sehemu ya eneo la Kanamai katika kaunti ya Kilifi itakosa umeme kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja jioni.