Waziri wa Kilimo Mithika Linturi aisuta NACADA kuorodhesha miraa kama dawa ya kulevya

Bw Linturi alikuwa akifika mbele ya kamati inayoongozwa na Seneta wa Tharaka Nithi Mwenda Gataya iliyokuwa ikizingatia Kanuni za Mazao (Miraa) 2023.

Muhtasari

• Alisema mapambano ya kutaka miraa kutambulika kuwa zao ni ya muda mrefu na inasikitisha kwamba waliopo ofisi ya Nacada wanapingana na watangulizi wao.

Tanzania yateketeza shamba la miraa.
Tanzania yateketeza shamba la miraa.
Image: STAR

Waziri wa Kilimo na Mifugo Mithika Linturi ameisuta Mamlaka ya Kitaifa ya Kampeni Dhidi ya Unywaji Pombe na Dawa za Kulevya (Nacada) kwa kuorodhesha zao la Miraa kama dawa ya kulevya, runinga ya NTV imeripoti.

 Waziri huyo alisema miraa na lahaja yake ya muguka imetambuliwa kama zao na Sheria ya Mazao, 2013, na akasema kuwa Nacada haiwezi kuchukua msimamo tofauti na mashirika mengine ya serikali kiholela.

Akitokea mbele ya kamati ya Seneti kuhusu Sheria jana, CS Linturi alimshutumu afisa mkuu mtendaji wa Nacada Victor Okioma kwa kupingana na watangulizi wake na serikali kwa kutangaza miraa kuwa dawa ya kulevya.

Aliteta kuwa waliokuwa vigogo wa Nacada akiwemo Dkt Frank Njenga na John Mututho hapo awali walikubali kwamba miraa ni zao na wala si dawa ya kulevya, lakini nafasi hiyo sasa imeondolewa na Bw Okioma.

"Nacada ni tapeli kwa kutoa misimamo isiyolingana kabisa kuhusiana na miraa. Dkt Njenga na Mututho walisema miraa si dawa na uuzaji wake unaweza kuidhinishwa lakini kutofautiana kunaletwa na mwenzao aliyepo sasa,” akasema Bw Linturi.

Bw Linturi alikuwa akifika mbele ya kamati inayoongozwa na Seneta wa Tharaka Nithi Mwenda Gataya iliyokuwa ikizingatia Kanuni za Mazao (Miraa) 2023, zinazolenga kukuza, kuendeleza na kudhibiti sekta ya miraa.

Alisema mapambano ya kutaka miraa kutambulika kuwa zao ni ya muda mrefu na inasikitisha kwamba waliopo ofisi ya Nacada wanapingana na watangulizi wao.

CS huyo alisema kuwa Sheria ya Dawa za Kulevya na Dawa za Kisaikolojia inayotegemewa na Nacada inaainisha tu cathinone na cathine, zinazotokana na zao hilo, kama dawa lakini si miraa katika hali yake ya asili.

"Tumepitia mengi kuona kemikali mbili zinazopatikana kwenye miraa, cathinone na cathine, zikiondolewa kuainishwa kama dawa katika sheria zetu na masuala hayo yameshughulikiwa," alisema.