Mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo ameuawa kwa kudungwa kisu baada ya ugomvi klabuni.
Wanafunzi wa Chuo hicho walipokea taarifa hizo za kuhuzunisha za kifo cha Abel Pchumba,mwenye umri wa miaka 21 anayejulikana na wengi kama Kiddo,alfajiri ya Alhamisi.
Katika risala rasmi ya ndani kutoka chuo kikuu, ilithibitishwa kuwa kisa hicho cha kusikitisha kilitokea jana jioni, na mwili wa marehemu kwa sasa uko katika hospitali ya Tabaka mjini Kisii.
Maelezo zaidi yanatarajiwa kutolewa na shule wakati uchunguzi ukiendelea.
Taarifa kutoka kwa marafiki wa karibu wa marehemu zinaeleza kuwa Pchumba alihusika katika ugomvi mbaya karibu na hosteli ya Adams, eneo la makazi ya wanafunzi lililopo nje ya chuo.
Inadaiwa alidungwa kisu na mtu anayejulikana, ambaye alikuwa rafiki yake. Mshukiwa alikamatwa na polisi muda mfupi baada ya tukio hilo.
Ugomvi huo, kama unavyoshuhudiwa na wengine, unaaminika kuibuka kutokana na mzozo wa malipo ya bili yao katika klabu ya eneo walilokuwa wametembelea hapo awali.
Kufuatia shambulio hilo, mtuhumiwa alikimbia eneo la tukio na kuomba hifadhi katika moja ya hosteli, ambapo alitoa taarifa kwa watu wanaomfahamu kuhusu tukio hilo.
Pchumba alipelekwa katika zahanati ya jirani na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Misheni ya Tabaka ambako alifariki.
Mkuu wa polisi wa Rongo Peter Okiringi alisema walimtia mbaroni mshukiwa aliyehusika na kifo cha mwanafuni huyo.
“Tunamuilia mshukiwa wa mkasa huu. Tunaendelea na uchunguzi ili kujua nia gani kabla hajafikishwa mahakamani,” alisema.
Mamlaka imesema kwa sasa inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo cha tukio hilo la kusikitisha, na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ipasavyo.