KPLC yavunja kimya baada ya usiku mrefu wa giza kuu kote nchini

Sehemu nyingi za Kenya hazikuwa na umeme Jumamosi usiku na KPLC ilikubali kulikuwa na tatizo.

Muhtasari

•KPLC imeendelea kuwafahamisha Wakenya kuhusiana na kukatika kwa umeme kulikokumba taifa Jumamosi usiku.

•Jumamosi usiku, mwendo wa saa mbili, taifa lilishuhudia kukatika kwa umeme katika maeneo mengi.

Kenya Power

Kampuni ya kusambaza umeme nchini Kenya (KPLC) imeendelea kuwafahamisha Wakenya kuhusiana na kukatika kwa umeme kulikokumba taifa Jumamosi usiku.

Katika taarifa ya mwisho iliyotolewa saa mwendo wa saa tano na dakika 57 usiku wa kuamkia Jumapili, KPLC ilibainisha kuwa umeme umerejeshwa katika sehemu nyingi za nchi.

Kampuni hiyo pia ilisema kuwa wanafanya kazi ya kurejesha umeme katika maeneo ambayo bado hayakuwa yamepata mwanga kufikia wakati wa kutoa taarifa.

"Tumerejesha usambazaji wa umeme katika sehemu nyingi za nchi huku sehemu nyingi za Central Rift, Nyanza Kusini na Nairobi pia zikiwa zimerejeshewa," KPLC ilisema katika taarifa.

Waliongeza, "Tumeanza kurejesha umeme kwa mkoa wa Pwani na maeneo mengine yaliyobaki. Taarifa ya mwisho itatolewa kwa wakati unaofaa."

Hapo awali, mwendo wa saa nne usiku wa kuamkia Jumapili, KPLC ilikuwa imeeleza kuwa umeme ulikuwa umerejeshwa katika maeneo kadhaa ya nchi ikiwa ni pamoja na sehemu za eneo la Mlima Kenya, Eneo la Magharibi na Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

"Urejesho wa stima kwa sehemu zilizobaki za nchi unaendelea vizuri," walisema.

Kampuni hiyo, wakati huo ilikuwa imewataka wateja wao kuwa na subira wanapofanya kazi ya kutatua tatizo hilo.

Jumamosi usiku, mwendo wa saa mbili, taifa lilishuhudia kukatika kwa umeme katika maeneo mengi.

KPLC ilikiri kukatika kwa umeme na ikaripoti kuwa wahandisi wao walikuwa wakifanya kazi kurejesha hali ya kawaida.

“Tunaomba radhi kwa wateja wetu kwa usumbufu uliojitokeza. Taarifa kuhusu maendeleo ya urejeshaji na sababu ya kukatika kwa umeme itatolewa baadaye,” KPLC ilisema.

Wakenya walikuwa wamezamia kwenye mitandao ya kijamii kuelezea kusikitishwa kwao na kampuni hiyo ya umeme baada ya kukatika Jumamosi usiku.