Haiti lazima: Bunge lapitisha pendekezo la kupelekwa kwa polisi 1000 nchini Haiti

Mapema mwezi jana, idara ya polisi, NPS ilitoa mwongozo wa jinsi idadi ya polisi 1000 itakavyopatikana, ikiwa ni kila kituo kupendekeza maafisa 2 wa polisi kote nchini.

Muhtasari

• Katika kura ya asubuhi siku ya Alhamisi, wabunge walipitisha ripoti ya kamati za pamoja ambayo ilikuwa imependekeza kwamba Bunge liidhinishe kutumwa kwa polisi Haiti.

Makurutu wa polisi
Makurutu wa polisi
Image: TWITTER// DCI

Wabunge katika bunge la kitaifa asubuhi ya Alhamisi walipitisha hoja inayolenga kupelekwa kwa maafisa 1000 nchini Haiti kwa ajili ya kuongoza oparesheni ya kurudisha Amani na usalama mitaani.

Katika kura ya asubuhi siku ya Alhamisi, wabunge walipitisha ripoti ya kamati za pamoja ambayo ilikuwa imependekeza kwamba Bunge liidhinishe kutumwa kwa polisi Haiti.

“Kamati baada ya kukagua wajibu wa Kenya kwa Umoja wa Mataifa, mfumo wake wa kisheria uliopo, mawasilisho kupitia ushirikishwaji wa umma na mawasilisho ya washikadau inapendekeza kwamba Bunge liidhinishe mapendekezo ya kutumwa kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi kwa Misheni ya Kimataifa ya Usaidizi wa Usalama (MSS) kwa Haiti chini ya masharti. ya Katiba,” timu ya pamoja ilipendekeza.

Hii ni baada ya serikali ya Kenya kusema kwamba ilikuwa radhi kuchangia katika usalama wa nchini hiyo ya Carrebean ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisumbuliwa na magenge hatari.

Kuitishwa kwa pendekezo hilo sasa kunatoa ruhusa kwa maafisa wa polisi kutolewa katika kila kituo cha polisi kote nchini ili kujenga timu ya angalau polisi 1000 katika misheni hiyo.

Uamuzi wa serikali kutuma wanajeshi hao umeonekana kuwa wa kutatanisha na tayari wakili alikuwa ameenda mahakamani akitaka kusimamisha kabisa kutumwa kwa wanajeshi hao.

Mapema mwezi jana, Radiojambo.co.ke ilielewa kwamba idara ya polisi NPS ilikuwa imetoa mwongozo wa jinsi maafisa hao 1000 watakavyopatikana kwa ajili ya misheni hiyo.

Mwongozo huo ulitaka kila afisa mkuu katika kila kituo cha polisi kote nchini kupendekeza angalau maafisa 2 kutoka kila kituo kote nchini ili kutengeneza kikosi cha maafisa 1,000 kwenda Haiti.