Raila ajuta kumsihi Tim Wanyonyi kumuachia Polycarp Igathe tikiti ya ugavana Nairobi

Kulingana na kinara huyo wa upinzani, muungano huo ulipoteza kiti hicho kwa sababu mgombea waliyemsimamisha hakutosha.

Muhtasari

• "Tulishinda Seneta, Mwakilishi wa Mwanamke, na kiti cha Urais, tunawezaje kupoteza kiti cha ugavana? Haiwezekani,” Odinga alisema.

Odinga akiwa na huzuni
Odinga akiwa na huzuni
Image: Maktaba

Kinara wa mrengo wa upinzani, Raila Odinga ameonyesha majuto yake kufuatia muungano wa Azimio la moja One Kenya kukosa kushinda wadhifa wa ugavana Nairobi katika uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka jana.

Akizungumza katika eneo la Westlands viungani mwa jiji la Nairobi, Odinga alisema kwamba mpaka leo hii hajawahi acha kujilimbikizia majuto ya kutomuidhinisha mbunge wa Westlands Tim Wanyonyi kuwania ugavana kumenyana na gavana wa sasa aliyeibuka mshindi Johnson Sakaja.

Odinga alisema kwamba anajuta kushawishiwa kumpa Polycarp Igathe tikiti ya Azimio kuwakilisha muungano huo kumenyana na Sakaja aliyependekezwa na Kenya Kwanza kupitia UDA kuwania ugavana katika jiji hilo linalotajwa kuwa kitovu cha uchumi wa Kenya.

“Najuta mwenyewe, niliambiwa nimwambie Tim aachie ngazi. Tim alikuwa mzuri vya kutosha, na akakubali. Tulitaka awe mgombea mwenza lakini alikataa. Alisema tumruhusu arejee Westlands,” Odinga alisema.

Kulingana na kinara huyo wa upinzani, muungano huo ulipoteza kiti hicho kwa sababu mgombea waliyemsimamisha hakutosha.

Katika hotuba yake, Odinga aliashiria kwamba walishinda kila kitu hadi yeye mwenyewe kudokeza kwamba alishinda urais.

"Tulishinda Seneta, Mwakilishi wa Mwanamke, na kiti cha Urais, tunawezaje kupoteza kiti cha ugavana? Haiwezekani,” Odinga alisema.

Katika kongamano hilohilo, Raila pia aliibua wasiwasi kuhusu kucheleweshwa kwa matokeo ya urais kwenye kidato cha 34-C na IEBC zaidi ya mwaka mmoja baada ya uchaguzi.

"Imepita mwaka mmoja, na matokeo ya urais bado hayajachapishwa kwenye Fomu 34-C. Hakuna aliyetoa maelezo ya kushindwa kutangaza matokeo kwenye gazeti la serikali. Hatuwezi kuendelea kuishi katika hali ya upotoshaji kila siku,” Raila alisema.

Matamshi ya Raila yalijiri siku moja baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Wafula Chebukati kusema kwamba Uchaguzi Mkuu wa 2022 ni wa kuaminika zaidi katika historia ya Kenya.