"Mjue kuna nuru gizani" Kalonzo ailalamikia KPLC kuongeza bei ya umeme

“Sababu ya gharama ya maisha kutoonekana katika ripoti ya kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa ni kwa sababu tulikubali kutokubaliana,” alisema Musyoka.

Muhtasari

• “Ongezeko la 16% la tokeni kwa @KenyaPower ni mzigo wa hivi punde usiokubalika kwa Wakenya," alisema.

Kalonzo Musyoka.
Kalonzo Musyoka.
Image: X

Kinara mwenza wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Kalonzo Musyoka ameonyesha kukerwa kwake na hatua ya hivi punde iliyochukuliwa na kampuni ya kusambaza umeme KPLC kwa kuongeza bei za bidhaa hiyo muhimu.

Kupitia ukurasa wake wa X, Musyoka alisema bei hizo mpya hazikubaliki na kuinyooshea serikali ya Kenya Kwanza kidole cha lawama kutokana na kile alisema ni kushindwa kuboresha maisha kwa Mkenya wa kawaida.

“Ongezeko la 16% la tokeni kwa @KenyaPower ni mzigo wa hivi punde usiokubalika kwa Wakenya waliochoka, wenye njaa na wenye hasira. Huu ni mfano uliosafishwa wa kutoweza kwa serikali ya KK kushughulikia gharama ya maisha,” Musyoka alisema.

Kiongozi huyo wa WIPER alisema kwamba serikali ya Ruto ina njama ya kuwatupa mamilioni ya Wakenya gizani lakini akasema kuwa bado hawataweza kwani kuna nuru gizani.

“Wanataka kutuacha gizani, lakini nawaambia, mjue kuna nuru gizani,” aliongeza.

Musyoka pia alisema kwamba jambo ambalo linafanya suala la bei za umeme kutoonekana kwenye mswada wa mazungumzo ya pande zote mbili ni kutokana na kwamba huenda walishindwa kuelewana au walielewana.

“Sababu ya gharama ya maisha kutoonekana katika ripoti ya kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa ni kwa sababu tulikubali kutokubaliana,” alisema.

Ikumbukwe Musyoka ndiye alikuwa anawakilisha upande wa upinzani katika mazungumzo hayo huku upande wa serikali ukiwakilishwa na mbunge wa Kikuyu ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge, Kimani Ichung’wah.