Kwa mara nyingine rais mstaafu Uhuru Kenyatta wamekutana na rais mrithi wake William Ruto katika hafla ya kuapishwa kwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi.
Wawili hao walionekana wakiwa wamesalimiana kwa furaha, jambo ambalo lilizua minong’ono kwenye mitandao ya kijamii ikizingatiwa kwamba wawili hao wamekuwa ni mahasimu wasioweza kuonana jicho kwa jicho tangu Ruto alipoapishwa kama rais.
Tshisekedi aliapishwa Jumamosi katika Uwanja wa Martyrs mjini Kinshasa.
Rais mteule Tshisekedi alipata zaidi ya asilimia 70 ya kura zote zilizopigwa wakati wa uchaguzi mkuu. Uchaguzi huo ulifanyika Desemba 2023 ambapo alipata kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.
Uhuru alihudhuria hafla hiyo kama Mwezeshaji wa Mchakato wa Amani wa Nairobi unaoongozwa na EAC. Rais Mstaafu alikaa mita chache kutoka kwa Ruto wakati wa kuapishwa kwa Tshisekedi.
Waliketi karibu na kila mmoja wakati wa kuapishwa kwa Rais Ruto Kasarani mnamo Septemba 13, 2022.
Wawili hao wamekuwa hawaonani macho kwa macho tangu Uhuru alipoamua kumuidhinisha Mkuu wa Azimio Raila Odinga kuwania urais badala ya Ruto ambaye awali aliahidi kuunga mkono Urais.
Kupeana mkono kati ya Uhuru na Ruto kumeibua hisia kutoka kwa Wakenya katika mtandao wa X baadhi wakisema kwamba kicheko na tabasamu lililodhihirika linafaa kumfungua macho kinara wa Azimio Raila Odinga ambaye wanahisi anachezewa shere.