Kunani? Safaricom yavunja kimya kuhusu tatizo la malipo ya Mpesa

Kampuni ya Safaricom imekiri kuwa kuna tatizo la kujirudia la huduma linaloathiri baadhi ya malipo ya Mpesa.

Muhtasari

•Katika taarifa ya siku ya Jumanne asubuhi, kampuni hiyo ilisema kwamba tatizo hilo kwa sasa linatatuliwa na timu ya kiufundi.

CEO PETER NDEGWA
Image: MAKTABA

Kampuni ya kutoa huduma za simu za mkononi ya Safaricom PLC imekiri kuwa kuna tatizo la kujirudia la huduma linaloathiri baadhi ya malipo ya Mpesa.

Katika taarifa ya siku ya Jumanne asubuhi, kampuni hiyo ilisema kwamba tatizo hilo kwa sasa linatatuliwa na timu ya kiufundi.

“Ndugu mteja, tunakumbwa na tatizo la huduma linalojirudia ambalo linaathiri baadhi ya malipo ya PayBill. Suala hili linatatuliwa na timu yetu ya kiufundi, tutawajulisha mara huduma za kawaida zitakaporejea,” Safaricom ilisema katika taarifa.

Waliongeza, “Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza. Asante kwa uvumilivu wako."

Tatizo lililoathiri malipo mengi muhimu ya mpesa yakiwemo malipo ya benki na ya umeme ( KPLC tokens) ilitokea Jumatatu jioni na kuzua malalamishi kutoka kwa umma.

Kampuni hiyo ilisema mnamo Jumatatu jioni kwamba tatizo hilo limetatuliwa lakini lilikuja kutokea tena usiku.

"Tulikumbana na usumbufu wa huduma kwa malipo ya PayBill ambao ulisababisha baadhi ya miamala kutokamilika kwa M-pesa," kampuni hiyo ilisema.

“Suala la kiufundi limetatuliwa na tunaendelea kufuatilia huduma kwa karibu. Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.”

Wakenya walitumia mitandao ya kijamii kuelezea masikitiko yao baada ya kujaribu bila mafanikio kulipa bili na huduma kwa kutumia bili ya malipo ya M-PESA. Huduma moja kuu ambayo ilikuwa imeathiriwa ni ununuzi wa tokeni kupitia Mpesa.