Walioathirika katika mkasa wa moto Embakasi watapata Sh5000 kila mmoja - Passaris

"Hawa wote ambao wamepatwa katika mkasa huu tunawapatia godoro, blanketi, mkate, soda na pia tutawapatia shilingi elfu 5 ili waweze kwenda nyumbani" Passaris alisema.

Muhtasari

• Mwanasiasa huyo alitoa maelezo ya jinsi kiwango hicho cha shilingi elfu 5 kinaweza kuwa cha maana kwa waathirika.

Mwakilishi wa wanawake Nairobi atoa msaada kwa waathirika wa moto Embakasi.
ESTHER PASSARIS// Mwakilishi wa wanawake Nairobi atoa msaada kwa waathirika wa moto Embakasi.
Image: Facebook

Mwakilishi wa kike wa kaunti ya Nairobi Esther Passaris ametoa hakikisho kwamba kila mmoja aliyeathirika katika mkasa wa moto huko Embakasi atapokezwa kitita cha shilingi elfu 5 kama malipo ya kwanza ya fidia kwa hasara walizozipata.

Akizungumza kupitia runinga ya NTV Kenya ambapo ilikuwa inapeperusha matangazo yao ya Adhuhuri kutoka katika hospitali ya Mama Lucy ambako mamia ya waathirika wanatibiwa, Passaris alisema kwamba tukio hilo ni la kustaajabisha sana na watu wengi wamekoseshwa makazi na wanahitaji msaada wa haraka.

“Tukio ambalo lilitokea usiku wa kuamkia leo, watu kama 280 hivi walichomwa moto na tayari 3 walipoteza maisha. Tunakumbuka zile familia ambazo zilipoteza wapendwa wao sasa sisi kama Women Rep tuko na NGAAF Fund, nimepigia CEO asubuhi na nikamwambia tutahitaji kutoa misaada,” Passaris alisema.

“Zile hela za majanga ambazo tunapewa ni milioni moja tu kwa mwaka na tayari zimeshakwisha kwani tumenunua godoro na tumehifadhi ili kukitokea visa kama hivi tunaweza kutoa msaada mara moja. Hawa wote ambao wamepatwa katika mkasa huu tunawapatia godoro, blanketi, mkate, soda na pia tutawapatia shilingi elfu 5 ili waweze kwenda nyumbani, unajua kila kitu sasa hivi kimechomeka,” aliongeza.

Mwanasiasa huyo alitoa maelezo ya jinsi kiwango hicho cha shilingi elfu 5 kinaweza kuwa cha maana kwa waathirika.

“Unajua hiyo elfu 5 inaweza kuwasaidia kupata mahali pa kwenda kuishi leo, kwa sababu sasa wanataka kuona pahali pa kulala na huo ndio msaada wa haraka ambao tunaweza kuwapatia. Kila wakati ambapo tuna janga kama hili tunatoa elfu 5 halafu pia tutaangalia jinsi tutaweza kupata mabati na vitu vingine, kwa sasa tumewapa kile cha kwenda kupata makao na cha kula,” aliongeza Zaidi.

Awali, Passaris alisitisha ziara yake ya kwenda Pwani ya Kenya na kufululiza moja kwa moja hadi katika eneo la tukio ili kuwafariji wanafamilia walioathirika.