Raila atoa Sh1 milioni kwa manusura wa moto Embakasi

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alitangaza Jumamosi kuwa Raila alimtumia pesa hizo kama sehemu ya mchango wake kwa waathiriwa.

Muhtasari

• Mbunge ambaye mkasa huo ulitokea katika eneo bunge lake alisema wanasiasa zaidi wanaoshirikiana na muungano wa Azimio pia wanachangia kitita hicho.

Moto Embakasi
Moto Embakasi
Image: COLLINS APUDO//THE STAR

Kinara wa upinzani Raila Odinga ametoa Sh1 milioni kusaidia walioathiriwa na mkasa wa gesi Embakasy.

Serikali ilisema lori lililokuwa limebeba mitungi ya gesi lililipuka Alhamisi usiku, na kuacha njia ya uharibifu baada ya moto mkubwa kuenea kwenye makazi yasiyo rasmi ya karibu.

"Jana (Alhamisi) mwendo wa saa 11:30 jioni, kulitokea mlipuko mkubwa eneo la Mradi, eneo la Embakasi, Kaunti ya Nairobi. Lori moja lililokuwa limesheheni gesi lililipuka na kuwasha moto mkubwa uliosambaa sana," alisema msemaji wa serikali Isaac Mwaura. .

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alitangaza Jumamosi kuwa Raila alimtumia pesa hizo kama sehemu ya mchango wake kwa waathiriwa.

Wakati huo huo, Babu alisema pia ametoa mchango wa kibinafsi wa Sh1 milioni kusaidia wote walioathiriwa na mlipuko wa Alhamisi usiku.

"Leo asubuhi H.E Baba Raila Amolo Odinga alinitumia Shilingi milioni 1 za Kenya kusaidia waathiriwa wa moto," Babu alisema kwenye akaunti yake rasmi ya X.

Mbunge ambaye mkasa huo ulitokea katika eneo bunge lake alisema wanasiasa zaidi wanaoshirikiana na muungano wa Azimio pia wanachangia kitita hicho.

''Isitoshe, nimechangia Sh1 milioni za ziada kwa lengo hili kuu la jumla ya Sh2 milioni. Viongozi wengine wa Azimio nao wanachangia katika hili,'' alisema Babu.

Mwaura mnamo Ijumaa alitembelea eneo la Embakasi lililoathiriwa na moto kufuatia mkasa huo na kutangaza kuwa watu watatu wamepoteza maisha yao.

Alisema serikali imejitolea kulipa kodi kwa familia zilizoathiriwa kwa miezi miwili wanapochukua vipande vyao ili kuanza maisha tena.

Akiwahutubia wakazi hao, Mwaura alisema kuwa serikali inashirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya na serikali ya kaunti ya Nairobi ili kuwaepusha na athari za moto uliotokea Alhamisi usiku.

Alitoa rambirambi zake kwa familia za wahasiriwa waliokufa kwa moto.

"Kufikia sasa, serikali imebaini kuwa watu watatu walifariki kutokana na moto huo na 280 ndio jumla ya walioathirika," Mwaura alisema.

Wazima moto walifanikiwa kuudhibiti moto huo mwendo wa saa 9:00 asubuhi siku ya Ijumaa, zaidi ya saa tisa baada ya moto huo kulipuka.

Mlipuko huo uliwasha "mpira mkubwa wa moto ulioenea sana", Mwaura alichapisha kwenye X.

Mlipuko huo uliwalazimisha wakazi wengi wa eneo hilo kulala nje huku nguzo kubwa za moshi mweusi ukifuka kutoka eneo hilo.