Chebukati ana haki ya kushikilia wadhifa wa jaji, asema Mudavadi

Mudavadi anamtetea Chebukati siku chache baada ya Raila Odinga kudai kwamba Ruto ana mpango wa kumteua kama Jaji Mkuu kabla ya uchaguzi wa 2027 kama njia ya kujihakikishia ushindi.

Muhtasari

• "Tume ya Huduma za Mahakama pia ni huru na ina haki ya kuajiri mtu yeyote aliyehitimu. Ni makosa kwa Azimio kuanza kubainisha ni nani JSC anafaa kuajiri," alisema.

Musalia Mudavadi
Musalia Mudavadi
Image: Facebook

Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi sasa anasema kwamba aliyekuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati ana haki ya kujipendekeza kwa nafasi ya jaji ikiwa anataka kufanya hivyo.

Akizungumza mjini Kakamega wakati wa ibada ya makanisa mbalimbali iliyohudhuriwa na Rais William Ruto, Mudavadi alisisitiza kuwa shughuli ya kuwaajiri watu hao itatekelezwa na Tume huru ya Huduma za Mahakama (JSC).

"Tume ya Huduma za Mahakama pia ni huru na ina haki ya kuajiri mtu yeyote aliyehitimu. Ni makosa kwa Azimio kuanza kubainisha ni nani JSC anafaa kuajiri," alisema.

Baada ya miaka sita ya utumishi Chebukati pamoja na makamishna wengine wawili wa zamani Abdi Guliye na Boya Molu waliondoka kwenye tume hiyo baada ya muda wao kukamilika.

Mudavadi alikuwa akikashifu matamshi yaliyotolewa na kiongozi wa Azimio Raila Odinga ambaye alimshutumu na kudai kuwa Mkuu wa Nchi alipanga kumwita Chebukati kama Jaji Mkuu kabla ya uchaguzi wa 2027.

Akihutubia wanahabari Ijumaa, chifu huyo wa Azimio alidai alifahamu kuhusu nia hiyo baada ya mkutano wa hivi majuzi wa Ikulu kati ya Watendaji wakiongozwa na Rais William Ruto na Idara ya Mahakama inayoongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome.

Kinara huyo wa upinzani pia alidai kuwa mkutano huo wa Ikulu ulikuwa sehemu moja tu katika mpango mkuu wa Rais Ruto wa kuwa na Mahakama rafiki.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati atateuliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa, huku Chebukati akiteuliwa kuwa Jaji Mkuu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027,” alidai.

Idara ya mahakama imepanga kuongezwa kwa bajeti kufuatia mazungumzo kati ya Rais Ruto na CJ Koome mwezi uliopita.

Bajeti hiyo itasaidia katika kuboresha utoaji wa huduma kwa ufanisi na mapambano dhidi ya rushwa.

Sehemu ya fedha hizo zitakwenda kwa ajili ya kuwapata majaji 36 ambapo 25 watakuwa wa Mahakama Kuu na 11 wa Mahakama ya Rufani.