Stephen Letoo aomboleza kifo cha ghafla cha PA wake Obed Kaizer maarufu 'Grand Muller'

Kifo chake cha ghafla kimeibua maswali mengi kuliko majibu, kwani mara ya mwisho alionekana mitandaoni ni siku 5 tu zilizopita.

Muhtasari

•  Hata hivyo, baadhi ya watu wa karibu naye walidai kwamba Kaizer alijisikia vibaya na alifariki muda mfupi kabla ya kuingizwa katika chumba cha kufanyiwa upasuaji.

Maarufu kama Grand Muller Kaizer
Obed Kaizer// Maarufu kama Grand Muller Kaizer
Image: Facebook

Mwanahabari wa runinga ya Citizen, Stephen Letoo ametupwa katika kipindi cha maombolezo kufuatia kifo cha rafiki wake wa karibu ambaye amefichua alikuwa kama msaidizi wa shughuli zake zote nje na uanahabari.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Letoo alisema rafiki huyo kwa jina Obed Kaizer maarufu kama Grand Muller ambaye alifuzu miaka michache iliyopita kutoka chuo kikuu cha Nairobi alifariki ghafla kwani mara ya mwisho kuzungumza na yeye, alikuwa sawa kabisa na buheri wa afya.

Letoo alimuomboleza kama moja ya nguzo yake muhimu ambayo imedondoka, akisema kwamba Kaizer alikuwa na kumbukumbu za hafla yake kuu ijayo mwezi Aprili, lakini pia ndiye alikuwa wakati mwingine anamsaidia katika kuendesha kurasa zake mitandaoni.

“Nguzo yangu moja imetoweka! Tulipozungumza mara ya mwisho alikuwa na furaha tele. Alikuwa na rekodi na kumbukumbu zangu zote pamoja na ile ya matukio yangu yote yanayokuja. Alisimamia mawasiliano yangu yote ya mitandao ya kijamii, alikuwa Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Nairobi. Pumzika kwa Power Kaizer,” Letoo aliandika kwa majonzi.

Taarifa za kijana huyo ambaye alikuwa mcheshi katika mitandao ya kijamii zilifika mitandaoni mapema Jumamosi huku chanzo cha kifo chake cha ghafla kikisalia kuwa kitendawili ambacho bado hakijateuliwa.

 Hata hivyo, baadhi ya watu wa karibu naye walidai kwamba Kaizer alijisikia vibaya na alifariki muda mfupi kabla ya kuingizwa katika chumba cha kufanyiwa upasuaji.

Watu mbali mbali katika mitandao ya kijamii wamemuomboleza kijana huyo aliyetajwa kuwa na umri wa miaka 26 ambaye kifo chake cha ghafla kimeibua maswali mengi kuliko majibu, kwani mara ya mwisho alionekana mitandaoni ni siku 5 tu zilizopita.