"Hakuna minisketi,tumbo-cut, crocs!" Chuo Kikuu cha Moi chatoa sheria kali kwa wanafunzi

Mkuu wa wanafunzi ameonya kuhusu hatua za kinidhamu kwa wanafunzi wote watakaobainika kukiuka miongozo ya uvaaji.

Muhtasari

•Uongozi wa shule hiyo ulisema kuwa umebaini kwa wasiwasi kuwa baadhi ya wanafunzi wake walikuwa wakivalia isivyofaa.

•Wahadhiri na wafanyikazi wengine wa chuo kikuu wameombwa kutohudumia wanafunzi ambao hawafuati kanuni zinazofaa za mavazi

Chuo Kikuu cha Moi - Eldoret
Image: Mathews Ndanyi (The Star)

Chuo Kikuu cha Moi kilicho mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu kimetoa mwongozo mpya wa uvaaji kwa wanafunzi wake.

Katika barua ya ndani kwa wanafunzi wote ambayo ilitolewa mnamo Februari 6, uongozi wa shule hiyo ulisema kuwa umebaini kwa wasiwasi kuwa baadhi ya wanafunzi wake walikuwa wakivalia isivyofaa.

"Napenda kuwafahamisha Kifungu cha 3.1.1 a,c,d, cha sheria na kanuni zinazosimamia maadili na nidhamu ya wanafunzi.

Wanafunzi wanatarajiwa kuvaa mavazi ya kujisitiri na yanayostahili. Hata hivyo, tumezingatia na kubainisha kwa wasiwasi uvaaji usio na adabu wa baadhi yenu," barua iliyotiwa saini na mkuu wa wanafunzi Alice C. Mutai ilisoma.

Mkuu huyo wa wanafunzi aliendelea kuorodhesha baadhi ya mavazi yanayovaliwa na wanafunzi ambayo taasisi hiyo inaona sio rasmi.

Mavazi hayo ni pamoja na, sketi ndogo au sketi ndogo kabisa, jeans zilizochanika au kuraruka au kupasuliwa, tumbo-cut, blauzi/nguo zilizokatwa chini, kaptula ndogo na nguo za uwazi au mavazi yanayoonyesha mikanda ya sidiria au t-shirt zisizo na mikono

Nyingine ni pamoja na, t-shirt zenye maandishi machafu, suruali na nguo zinazofichua kifua, slippers, crocs na viatu vyote vya plastiki.

"Si mavazi rasmi na hayafai kuvaliwa chuo kikuu," memo ilisoma.

Mkuu huyo alionya kuhusu hatua za kinidhamu kwa wanafunzi wote watakaobainika kukiuka miongozo ya uvaaji.

Wahadhiri na wafanyikazi wengine wa chuo kikuu pia waliombwa kutohudumia wanafunzi wowote ambao hawafuati kanuni zinazofaa za mavazi.

"Hii ni kwa hivyo kuwataka wanafunzi wote wavae kwa heshima na wafanyikazi wanaombwa KUTOWAhudumia wanafunzi ambao wamevalia visivyo," memo ilisoma.