Embu: Mwalimu ajiua na kuacha waraka kuzikwa siku ya Valentino, ex wake kusoma eulogy

Kwa maelezo yake kwenye Facebook, mwalimu huyo alisema aliamua kujiua kwa kutemwa na mpenzi wake wa zamani na kutaka azikwe siku ya wapendanao na huyo Ex wake kupewa ruhusa ya kusoma eulogy yake.

Muhtasari

• Barua ya kujitoa mhanga inayoaminika kuandikwa na Mwaniki ilipatikana ndani ya nyumba hiyo.

• Katika maelezo hayo, marehemu alieleza kwa nini aliamua kukatisha maisha yake.

Picha ya maktaba ya gari la Polisi la Kitengela katika eneo la uhalifu hapo awali.
Image: MAKTABA

Mwalimu mmoja wa kiume katika kaunti ya Embu amewashangaza wengi baada ya kujitoa uhai kisa kukataliwa na mpenzi wake wa zamani huku akiacha barua ya jinsi atakavyozikwa.

Kwa mujibu wa maelezo yake kwenye Facebook, Dennis Mwaniki maarufu kama Mkono, mwenye umri wa miaka 32 alianza kwa kuwaalika marafiki zake kwa shughuli yake kuu itakayofanyika siku ya wapendanao, Februari 14.

Bila kujua, kumbe alikuwa anatoa mwaliko kwa watu kuhudhuria mazishi yake kwani alikuwa tayari ameratibu kujitoa uhai kisa kukataliwa na aliyekuwa mpenzi wake.

"Wajumbe wa Jioni mkiwa na msongo wa mawazo mnahitaji tu rafiki mmoja wa kushiriki naye, wakati huo huo nawaalika kwenye shughuli yangu tarehe 14/2/2024 karibu wote."

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ndogo ya Mbeere Kaskazini Eric Yego alisema MCA wa Nthawa Sammy Tito alitoa ripoti katika Kituo cha Polisi cha Siakago kwamba mwanamume mmoja hakuwa akipokea simu kutoka kwa marafiki na familia na alikuwa amejifungia ndani ya nyumba yake katika kijiji cha Nthangariri.

Yego alisema polisi walivunja mlango ili kuingia ndani ya nyumba hiyo na walimpata Mwaniki akiwa amekufa juu ya kitanda chake bila majeraha yoyote ya mwili isipokuwa damu na vitu vyeupe vinavyotoka puani.

Barua ya kujitoa mhanga inayoaminika kuandikwa na Mwaniki ilipatikana ndani ya nyumba hiyo. Katika maelezo hayo, marehemu alieleza kwa nini aliamua kukatisha maisha yake.

Aliagiza kwamba mazishi yake yafanyike Februari 14. Mwaniki alionyesha katika noti hiyo nambari ya simu ya mwanamke ambaye alimwagiza asome ujumbe wake.