Rais William Ruto amemuomboleza bingwa wa dunia wa mbio za marathoni, Mkenya Kelvin Kiptum ambaye alipoteza maisha katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea kwenye barabara ya Eldoret-Kaptagat siku ya Jumapili usiku.
Kiptum ,24, na kocha wake raia wa Rwanda Gervais Hakizimana walifariki papo hapo kufuatia ajali mbaya iliyotokea umbali mfupi sana kutoka kijiji chake cha Chepsamo, magharibi mwa Kenya. Abiria wa kike aliyekuwa pamoja nao hata hivyo alinusurika na majeraha na kukimbizwa katika hospitali ya Racecourse mjini Eldoret huku miili ya Kiptum na mkufunzi wake ikipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Moi huku uchunguzi ukianza.
Huku akimuomboleza mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia ya Marathon, rais alimtaja kama nyota aliyevunja vizuizi ili kupata rekodi hiyo ya marathon.
“Kelvin Kiptum alikuwa nyota. Bila shaka ni mmoja wa wanamichezo bora zaidi duniani waliovunja vizuizi ili kupata rekodi ya mbio za marathon,” Rais Ruto aliomboleza.
Aliongeza, "Alikuwa na umri wa miaka 24 tu, kama shujaa, alishinda Valencia, Chicago, London na katika mashindano mengine ya juu. Nguvu zake za kiakili na nidhamu hazilinganishwi. Kiptum ilikuwa mustakabali wetu.”
Amri jeshi mkuu alibainisha kwamba licha ya kufariki akiwa na umri mdogo sana, marehemu Kiptum ameacha alama kubwa sana duniani.
Pia alichukua fursa hiyo kuifariji familia ya bingwa huyo wa mbio za marathon na wadau wote wa tasnia ya michezo.
"Mwanaspoti wa ajabu ameacha alama ya ajabu duniani. Mawazo yetu yako kwa familia na udugu wa michezo. Pumzika kwa Amani,” alisema.
Kiptum alivunja rekodi ya dunia ya marathon mwezi Oktoba, mwaka jana alipokimbia kwa masaa 2:00:35 katika Chicago Marathon, na kuwa mwanariadha wa kwanza kukimbia marathon chini ya saa mbili na dakika moja, na kuchukua sekunde 34 chini ya rekodi ya awali ya Mkenya mwenzake Eliud Kipchoge.
Alama yake ya mbio za dunia iliidhinishwa wiki iliyopita tu na shirikisho la kimataifa la Riadha Duniani, na alikuwa akijiandaa kufungua msimu wake mpya katika mbio za Rotterdam Marathon mnamo Aprili 14 mwaka huu kabla ya kujiunga na timu ya Kenya kwa Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.
Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wameendelea kumuomboleza marehemu Kiptum kihisia na kueleza mshtuko wao kutokana na kifo chake cha ghafla.