Mwakilishi wa wadi ya Kileleswa ambaye pia ni mwanachama wa kudumu wa chama cha ODM, Robert Alai ametoa maoni yake kuhusu jinsi wafuasi wengi wa chama hicho watajipanga mbele ya uchaguzi wa 2027 – iwapo kiongozi wao Raila Odinga hatokuwa debeni.
Alai kupitia ukurasa wake wa X alidai kwamba ikiwa Odinga hatokuwa debeni, kwa dhana kwamba atapata kiti cha kuwa rais wa tume ya muungano wa Afrika Januari mwaka ujao, basi wafuasi wengi wa ODM hawatomuona Kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka kama chaguo bora.
MCA huyo wa ODM alisema kwamba wafuasi wengi wa ODM wataonelea bora kumpigia Ruto kura kuliko kumpigia Kalonzo ambaye atakuwa amesalia kama mgombea wa urais kutoka muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, baada ya Raila kwenda AU.
“Ngoja nikuambie kwa uhakika sana. Ikiwa Baba [Raila Odinga] hatakuwa katika kinyang'anyiro cha 2027 na ikitolewa kati ya Kalonzo na Ruto, wafuasi wa ODM wangemfuata Ruto kwa urahisi. Wafuasi wa ODM wangemwamini Ruto kuhusu Kalonzo SIKU YOYOTE,” Alai alisema.
Mwanablogu huyo aliyegeuka mwanasiasa alisema kwamba ukweli kama huo aghalabu unamkera sana rais mstaafu Uhuru Kenyatta na naibu wa rais wa sasa Rigathi Gachagua lakini akasema huo utakuwa ukweli ambao watafaa kuanza kuuzoea kuanzia Janauri mwaka kesho endapo Odinga atafanikiwa kutwaa nafasi ya kuongoza tume ya umoja wa Afrika, AU-C.
“Ninajua kuwa Rigathi Gachagua na Uhuru wanachukia jambo hili kuliko mtu mwingine yeyote lakini huo ndio ukweli,” aliongeza.
Alai alitoa maoni yake saa chache baada ya Ruto na Raila kukutana nyumbani kwa rais wa Uganda Yoweri Museveni kujadili miongoni mwa masuala mengi, jinsi ya kumsaidia Odinga kutwaa nafasi ya urais AU-C.