Magavana wenye kaunti zenye visa vingi vya mimba za utotoni wapewa kadi nyekundu

Pia KHRC ilimtaka gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka kutengua agizo lake kwamba wasichana waliopachikwa mimba wasiruhusiwe kurudi shuleni.

Muhtasari

• Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa visa 452 huku Kakamega ikiwa ya pili kwa visa 328, Bungoma visa 294, Nakuru visa 283.

KHRC yatoa kadi nyekundu kwa kaunti zenye visa vingi vya mimba za utotoni
KHRC yatoa kadi nyekundu kwa kaunti zenye visa vingi vya mimba za utotoni
Image: Screengrab

Magavana wa kaunti kumi pamoja na waziri wa afya Susan Nakhumincha wameonyeshwa kadi nyekundu ya tume ya kutetea haki za kibinadamu KHRC kutokana na ongezeko la visa vya mimba za utotoni katika kaunti na idara zao.

KHRC ilitoa ripoti Alhamisi kwamba kaunti 10 zinaongoza katika visa vya mimba za utotoni, Nairobi ikiwa kileleni huku nafasi ya kumi ikiwa inashikiliwa na kaunti ya Narok.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa visa 452 huku Kakamega ikiwa ya pili kwa visa 328, Bungoma visa 294, Nakuru visa 283.

Kaunti zingine ambazo magavana wao walipewa kadi nyekundu na KKHRC ni pamoja na Kilifi yenye visa 224, Meru visa 206, Kisii visa 192, Machakos visa 178 na Narok visa 176.

KHRC pia imemkashifu Katibu wa waziri wa Afya Susan Nakhumicha kwa kile wanachodai kushindwa kuchukua hatua zinazoonekana na za kimaendeleo kushughulikia tatizo la mimba za utotoni.

“Tumetoa kadi nyekundu kwa Nairobi, Johnson Sakaja (Kakamega), Kenneth Lusaka (Bungoma), Fernades Barasa (Kakamega), Susan Kihika (Nakuru), Waving Ndeti Machakos, Kimani Wamatangi (Kiambu), Gideon Mung’aro (Kilifi), Kawira Mwangaza (Meru), Simba Arati (Kisii) na Patrick Ole Ntutu wa Narok,” Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa KHRC Davis Malombe alisema.

Kulingana na Utafiti wa Demografia na Afya nchini Kenya wa 2022, kaunti hizo 20 zilikuwa na idadi kubwa zaidi ya mimba zilizoripotiwa miongoni mwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 10 na 19.