Vihiga: Mama wa miaka 59 azirai na kufariki wakati wa ibada ya kesha

Muumini huyo alizimia asubuhi na mapema katika kanisa hilo linalojulikana kwa jina la Jesus Power, huku juhudi za waumini kumsaidia zikishindikana.

Muhtasari

• Mhudumu wa hospitali ya kibinafsi ambaye aliitwa kwenye eneo la tukio alithibitisha kuwa mwanamke huyo alikuwa tayari amefariki.

crime scene 1
crime scene 1

Huzuni na vilio vilitanda katika kanisa la Jesus Power, eneo la Sabatia kaunti ya Vihiga baada ya mama mmoja mwenye umri wa miaka 59 kudaiwa kuzirai na kufariki dunia baadae wakati wa ibada ya kesha mapema Jumamosi alfajiri.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka kaunti hiyo, alizimia asubuhi na mapema katika kanisa hilo linalojulikana kwa jina la Jesus Power, huku juhudi za waumini kumsaidia zikishindikana.

Mhudumu wa hospitali ya kibinafsi ambaye aliitwa kwenye eneo la tukio alithibitisha kuwa mwanamke huyo alikuwa tayari amefariki.

Maafisa wa polisi waliarifiwa na kufika eneo la tukio ambapo wameuhamisha mwili wa marehemu hadi chumba cha kuhifadhia maiti.

Aidha chifu huyo alieleza kuwa familia ya marehemu ilithibitisha kuwa mwanamke huyo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Pumu hali inayoshukiwa kusababisha kifo chake.

Mwili wa muumini huyo ulipelekwa katika makafani na uchunguzi kuanzishwa ili kubaini chanzo halisi cha kifo chake.