Chuo Kikuu cha Kenyatta kinaendelea kuwaomboleza wanafunzi kumi na mmoja waliofariki katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea Voi mapema wiki hii.
Wakati wanafunzi na wafanyikazi wakijaribu kukubaliana na tukio hilo la kusikitisha, taasisi hiyo imezindua njia mbalimbali ambazo wataonyesha heshima kwa walioaga.
Siku ya Jumatano jioni, wanafunzi na wafanyakazi walikusanyika pamoja kuwasha mishumaa kama njia ya kuwakumbuka vijana kumi na mmoja ambao maisha yao yalikatizwa na ajali hiyo.
“Jioni hii, Udugu wa Chuo Kikuu cha Kenyatta unakusanyika kwa mshikamano kwa mkesha wa kuwasha mishumaa kwa heshima ya wanafunzi walioaga katika ajali mbaya ya Maungu.
Mioyo yetu inawaendea familia na marafiki zao. Wacha kumbukumbu zao ziishi milele,” KU ilisema katika taarifa.
Tukio hilo lilifanyika katika Bishop Square na maelfu walijitokeza katika hafla iliyojaa hisia.
Mapema siku hiyo, wasimamizi walikuwa wametangaza kuwa kengele maalum itapigwa mwendo wa saa saba mchana na dakika ya kimya pia itazingatiwa.
“Saa saba kamili mchana, kengele ya Campanile italia kwa dakika moja kwa siku tatu zijazo kuanzia leo (Jumatano). Tunawaomba wafanyikazi wote na wanafunzi kunyamaza kwa dakika moja kuwakumbuka wanafunzi wetu walioaga," taasisi hiyo ilitangaza.
Masomo katika chuo kikuu hicho pia yamesimamishwa kwa siku tatu ili kuruhusu wanafunzi na wafanyikazi kuomboleza wenzao.
Kusimamishwa kwa masomo kulianza Jumatano hadi Ijumaa wiki hii.
‘Kufuatia mkasa huu mkubwa, Menejimenti ya chuo kikuu imeamua kusimamisha masomo yote kwa siku tatu kuanzia Jumatano tarehe 20 Machi 2024 ili kutuwezesha kuwaomboleza wanafunzi wetu wapendwa,” taarifa ya Jumanne iliyotiwa saini na msaidizi wa naibu chansela Prof. Waceke Wanjohi ilisoma.
Taasisi hiyo ilifichua kuwa ajali hiyo ilihusisha wanafunzi kutoka idara ya usimamizi wa afya na habari katika Shule ya Sayansi ya Afya.
Ilisema pamoja na wanafunzi kumi na mmoja waliopoteza maisha, wengine kumi na moja walijeruhiwa vibaya huku 16 wakipata majeraha madogo.
"Mipango inafanywa kusafirisha miili ya wanafunzi kumi na mmoja (11) hadi Mochari ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kando ya Thika Super Highway," taasisi hiyo ilisema.
Prof Waceke pia alifichua kuwa taasisi hiyo imetenga dawati la usaidizi ili kutoa usaidizi na pia kujibu maswali kuhusu ajali hiyo.