Mpango wa Boy Child haufadhiliwi na pesa za mlipakodi-Dorcas Rigathi

Alisisitiza kuwa mradi huo unafadhiliwa na ubia kutoka kwa watu wema na wafadhili.

Muhtasari
  • Akizungumza akiwa kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Dorcas alieleza kuwa inagharimu wastani wa Ksh80,000 kila mwezi kumrekebisha mtu mmoja.
Mama Dorcas Gachagua
Mama Dorcas Gachagua
Image: Facebook

Mke wa naibu Rais Rigathi Gachagua, Dorcas Rigathi mnamo Alhamisi, Machi 28, alifichua kwamba inagharimu mkono na mguu kufadhili mpango wake wa kuwawezesha watoto wa kiume ambao unalenga kuwarekebisha vijana wanaokabiliana na ulevi na dawa za kulevya.

Akizungumza akiwa kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Dorcas alieleza kuwa inagharimu wastani wa Ksh80,000 kila mwezi kumrekebisha mtu mmoja.

Alisema kuwa mtu huyo anaweza kuhitimu kutoka vituo vyake vya ukarabati baada ya miaka miwili.

Kulingana naye, taasisi yake iko mbioni kusajili maelfu ya vijana kote nchini ambao wameingia kwenye uraibu.

"Kwa sasa, tuna wafadhili ambao wako tayari kufadhili miradi hii. Wengine hutoa fedha, wengine bidhaa za kimwili. Mtu wa ukarabati anaweza kutumia kati ya Ksh40,000 hadi Ksh80,000 kila mwezi, ni ghali sana na wengine hutumia karibu miaka 2 katika taasisi hiyo," Dorcas alisema.

Dorcas alifafanua kuwa mpango wa Boychild haufadhiliwi na pesa za walipa kodi, kinyume na imani maarufu.

Alisisitiza kuwa mradi huo unafadhiliwa na ubia kutoka kwa watu wema na wafadhili.

"Hakuna fedha zilizotengwa na serikali. Hatuna bajeti ambayo itachangia maendeleo ya ukarabati kwa sababu kazi hii haijawahi kufanywa na tawala zilizopita," alifafanua.

"Sasa baada ya kuchukua madaraka, ni jambo ambalo limeangaziwa na tumeona ukubwa wa uharibifu ambao ulikuwa umesababisha katika jamii."

Akihutubia vita vya Naibu Rais Rigathi Gachagua dhidi ya pombe haramu katika eneo la Mlima Kenya, Bibi wa Pili alimsifu mwenzi wake kwa kuchukua jukumu kuu katika vita dhidi ya tabia mbaya inayoharibu vijana katika jamii.

"Halali, anaamka mapema kumrekebisha mtoto wa kiume na hilo ndilo jukumu lake la baba na kiongozi. Jukumu la kiongozi ni kuwatumikia wananchi," alifichua.