Mwanamke akamatwa JKIA baada ya kupatikana ameficha kokeini kwenye sehemu za siri

Alitiwa mbaroni baada ya ukaguzi wa mwili kufichua vitu vya kutiliwa shaka vilivyofichwa kwenye sehemu za siri.

Muhtasari

•Mshukiwa alikamatwa na kuzuiliwa katika seli ya polisi  alipokuwa akijaribu kutoroka ukaguzi wa usalama katika uwanja wa ndege.

•Polisi walimhoji mshukiwa ambapo alifichua kuwa alikuwa ameajiriwa kufanya kazi hiyo na raia wa Uganda aliyekuwa akiishi Nairobi.

Washukiwa watano walikamatwa kwa madai ya ulanguzi wa Kokeini
Image: TWITTER// DCI

Mwanamke aliyedaiwa kujaribu kujaribu kusafirisha gramu 600 za kokeini kutoka Kenya hadi nchini Madagscar alikamatwa Jumanne usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta alipokuwa akijaribu kuondoka nchini.

Damaris Adhiambo mwenye umri wa miaka 32 alikamatwa na kuzuiliwa katika seli ya polisi mwendo wa saa nne unusu usiku wa Jumanne alipokuwa akijaribu kutoroka ukaguzi wa usalama katika uwanja wa ndege.

DCI imeripoti kuwa mshukiwa alizuiliwa katika eneo la ukaguzi wa usalama alipokuwa akikaribia kupanda ndege yake kuelekea Madagaska baada ya ukaguzi wa mwili kufichua vitu vya kutiliwa shaka vilivyofichwa kwenye sehemu za siri.

"Hii ilizua uchunguzi wa haraka ambao uligundua gramu 600 ya dawa hiyo ya kulevya sana iligunduliwa. Ukaguzi uliofanywa kwenye bidhaa iliyopatikana ulionyesha kuwa ni bidhaa ya kokeini,” DCI ilisema kwenye taarifa Jumatano.

Kufuatia kukamatwa, polisi walimhoji mshukiwa ambapo alifichua kuwa alikuwa ameajiriwa kufanya kazi hiyo na raia wa Uganda aliyekuwa akiishi Nairobi.

Maafisa wa upelelezi walimtafuta mshukiwa mwingine, Bi Harriet Asaba na kumpata katika CBD CBD ambapo walimkamata pia.

Mshukiwa huyo baadaye aliwaongoza maafisa hao hadi afisi yake ambapo vidonge vingine 33 vya kokeini vilipatikana.

Watuhumiwa wengine watatu; Shirah Nangozi kutoka Uganda, Esther Wanjiru na Sophia Kathambi, walipatikana katika eneo la uhalifu na kukamatwa.

"Kipimo cha dhahania cha bidhaa ya pili pia kilithibitishwa kuwa na kokeini, yenye uzito wa takriban gramu 396," DCI ilisema.

Maafisa wa upelelezi wameeleza kuwa uchunguzi zaidi unafanywa ili kumsaka mtu aliyekusudiwa kupokea dawa hiyo nchini Madagascar.

Wakati huo huo, washukiwa watano waliokamatwa wamezuiliwa katika seli za polisi ambapo wanahojiwa ili kusaidia uchunguzi.